Zaburi 99

Open Word Bible

BWANA ni Mfalme; mataifa na yatetemeke! Ameketi juu ya makerubi kama juu ya kiti cha enzi; nchi na itikisike! Katika Sayuni BWANA ni mkuu; yeye yuko juu sana ya mataifa yote. Mataifa na yalishukuru jina lako, kuu na la kutisha. Yeye ni mtakatifu! Ee Mfalme mwenye nguvu unayependa haki, ni wewe uliyeuweka usawa imara; umetenda yaliyo ya haki na ya kweli katika Yakobo. Mwinueni juu BWANA Mungu wetu, msujudu mbele ya kiti chake cha miguu. Yeye ni mtakatifu! Kati ya makuhani wake walikuwa Musa na Haruni, na kati ya wale walioliitia jina lake alikuwa Samweli; walimlilia BWANA, naye akawajibu. Kutoka katika nguzo ya wingu alizungumza nao; walishika maagizo aliyoyaweka na kanuni aliyowapa. Ee BWANA Mungu wetu, ni wewe uliyewajibu. Kwao ulikuwa Mungu anayesamehe, lakini pia uliyeadhibu makosa yao. Mwinueni juu BWANA Mungu wetu, msujudu juu ya mlima wake mtakatifu, kwa sababu BWANA Mungu wetu ni mtakatifu.

Zaburi

Fungua msomaji shirikishi ili kubadilisha tafsiri, kurekebisha herufi, na kutia alama mistari — au vinjari mistari kwa mada.

Manukuu ya Maandiko yametoka katika Open Word Bible, ambayo iko katika uwanja wa umma.