Zaburi 36

Neno: Kiswahili Contemporary Version

Kuna neno moyoni mwangu kuhusu hali ya dhambi ya mwovu. Hakuna hofu ya Mungu mbele ya macho yake.

Kwa kuwa machoni pake mwenyewe hujisifu mno hata hawezi kugundua au kuichukia dhambi yake.

Maneno ya kinywa chake ni maovu na ya udanganyifu, ameacha kuwa mwenye hekima na kutenda mema.

Hata kitandani mwake hupanga hila mbaya, hujitia katika njia ya dhambi na hakatai lililo baya.

Upendo wako, Ee Bwana, unafika hadi mbinguni, uaminifu wako hadi kwenye anga.

Haki yako ni kama milima mikubwa, hukumu zako ni kama kilindi kikuu. Ee Bwana, wewe huwahifadhi mwanadamu na mnyama.

Upendo wako usiokoma ni wa thamani mno! Watu wakuu na wadogo hujificha uvulini wa mbawa zako.

Wanajifurahisha katika wingi nyumbani mwako, nawe utawanywesha katika mto wa furaha zako.

Kuwa pamoja nawe ni kijito cha uzima, katika nuru yako twaona nuru.

Dumisha upendo wako kwa wale wanaokujua wewe, haki yako kwa wale walio wanyofu wa moyo.

Mguu wa mwenye kiburi usije dhidi yangu, wala mkono wa mwovu usinifukuze.

Angalia jinsi watenda mabaya walivyoanguka: wametupwa chini, hawawezi kuinuka!

Zaburi

Fungua msomaji shirikishi ili kubadilisha tafsiri, kurekebisha herufi, na kutia alama mistari — au vinjari mistari kwa mada.

Neno: Bibilia Takatifu — Kiswahili Contemporary Version. Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. Used under the Biblica Open (Toleo Wazi) License. · Biblica Open License