Zaburi 32

Neno: Kiswahili Contemporary Version

Heri mtu yule ambaye amesamehewa makosa yake, ambaye dhambi zake zimefunikwa.

Heri mtu yule ambaye Bwana hamhesabii dhambi, na ambaye rohoni mwake hamna udanganyifu.

Niliponyamaza, mifupa yangu ilichakaa kwa kulia kwa maumivu makali mchana kutwa.

Usiku na mchana mkono wako ulinilemea, nguvu zangu zilinyonywa kama vile katika joto la kiangazi.

Kisha nilikujulisha dhambi yangu wala sikuficha uovu wangu. Nilisema, “Nitaungama makosa yangu kwa Bwana.” Ndipo uliponisamehe hatia ya dhambi yangu.

Kwa hiyo kila mtu mcha Mungu akuombe wakati unapopatikana, hakika maji makuu yatakapofurika hayatamfikia yeye.

Wewe ndiwe mahali pangu pa kujificha, utaniepusha na taabu na kunizunguka kwa nyimbo za wokovu.

Nitakufundisha na kukuonyesha njia utakayoiendea; nitakushauri na kukuangalia.

Usiwe kama farasi au nyumbu wasio na akili, ambao ni lazima waongozwe kwa lijamu na hatamu la sivyo hawatakukaribia.

Mtu mwovu ana taabu nyingi, bali upendo usio na kikomo wa Bwana unamzunguka mtu anayemtumaini.

Shangilieni katika Bwana na mfurahi, enyi wenye haki! Imbeni, nyote mlio wanyofu wa moyo!

Zaburi

Fungua msomaji shirikishi ili kubadilisha tafsiri, kurekebisha herufi, na kutia alama mistari — au vinjari mistari kwa mada.

Neno: Bibilia Takatifu — Kiswahili Contemporary Version. Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. Used under the Biblica Open (Toleo Wazi) License. · Biblica Open License