Zaburi 63

Neno: Kiswahili Contemporary Version

1Ee Mungu, wewe ni Mungu wangu, nakutafuta kwa moyo wote; nafsi yangu inakuonea kiu, mwili wangu unakuonea wewe shauku, katika nchi kame na iliyochoka mahali ambapo hapana maji.

2Nimekuona katika mahali patakatifu na kuuona uwezo wako na utukufu wako.

3Kwa sababu upendo wako ni bora kuliko uhai, midomo yangu itakuadhimisha.

4Nitakusifu siku zote za maisha yangu, na kwa jina lako nitainua mikono yangu.

5Nafsi yangu itatoshelezwa kama kwa wingi wa vyakula; kwa midomo iimbayo kinywa changu kitakusifu wewe.

6Kitandani mwangu ninakukumbuka wewe, ninawaza juu yako makesha yote ya usiku.

7Kwa sababu wewe ndiwe msaada wangu, chini ya uvuli wa mbawa zako naimba.

8Nafsi yangu inaambatana nawe, mkono wako wa kuume hunishika.

9Wale wanaotafuta uhai wangu wataharibiwa, watakwenda chini kwenye vilindi vya dunia.

10Watatolewa wafe kwa upanga, nao watakuwa chakula cha mbweha.

11Bali mfalme atafurahi katika Mungu, wale wote waapao kwa jina la Mungu watamsifu, bali vinywa vya waongo vitanyamazishwa.

Zaburi

Open the interactive reader to switch translations, adjust type, and mark verses — or browse verses by topic.

Neno: Bibilia Takatifu — Kiswahili Contemporary Version. Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. Used under the Biblica Open (Toleo Wazi) License. · Biblica Open License