Zaburi 79

Neno: Kiswahili Contemporary Version

1Ee Mungu, mataifa yameuvamia urithi wako, wamelinajisi Hekalu lako takatifu, wameifanya Yerusalemu kuwa magofu.

2Wametoa maiti za watumishi kuwa chakula cha ndege wa angani na nyama ya watakatifu wako kwa wanyama wa nchi.

3Wamemwaga damu kama maji kuzunguka Yerusalemu yote, wala hakuna yeyote wa kuwazika.

4Tumekuwa kitu cha aibu kwa jirani zetu, cha dharau na mzaha kwa wale wanaotuzunguka.

5Hata lini, Ee Bwana? Je, wewe utakasirika milele? Wivu wako utawaka kama moto hadi lini?

6Mwaga ghadhabu yako kwa mataifa yasiyokukubali, juu ya falme za hao wasioliitia jina lako,

7kwa maana wamemrarua Yakobo na kuharibu nchi ya makao yake.

8Usituhesabie dhambi za baba zetu, huruma yako na itujie hima, kwa maana tu wahitaji mno.

9Ee Mungu Mwokozi wetu, utusaidie, kwa ajili ya utukufu wa jina lako; tuokoe na kutusamehe dhambi zetu kwa ajili ya jina lako.

10Kwa nini mataifa waseme, “Yuko wapi Mungu wenu?” Mbele ya macho yetu, dhihirisha kati ya mataifa kwamba unalipiza kisasi damu iliyomwagwa ya watumishi wako.

11Kilio cha huzuni cha wafungwa kifike mbele zako; kwa nguvu za mkono wako hifadhi wale waliohukumiwa kufa.

12Walipize jirani zetu mara saba vifuani mwao aibu walizovurumisha juu yako, Ee Bwana.

13Ndipo sisi watu wako, kondoo wa malisho yako, tutakusifu milele; toka kizazi hadi kizazi tutasimulia sifa zako.

Zaburi

Open the interactive reader to switch translations, adjust type, and mark verses — or browse verses by topic.

Neno: Bibilia Takatifu — Kiswahili Contemporary Version. Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. Used under the Biblica Open (Toleo Wazi) License. · Biblica Open License