Zaburi 14

Neno: Kiswahili Contemporary Version

1Mpumbavu anasema moyoni mwake, “Hakuna Mungu.” Wameharibika, matendo yao ni maovu kabisa; hakuna hata mmoja atendaye mema.

2Bwana anawachungulia wanadamu chini kutoka mbinguni aone kama wako wenye akili, wowote wanaomtafuta Mungu.

3Wote wamepotoka, wameharibika wote pamoja, hakuna atendaye mema. Naam, hakuna hata mmoja!

4Je, watendao mabaya kamwe hawatajifunza: wale ambao huwala watu wangu kama watu walavyo mkate, hao ambao hawamwiti Bwana?

5Wako hapo, wameingiwa na hofu kuu, maana Mungu yupo pamoja na wenye haki.

6Ninyi watenda mabaya mnakwamisha mipango ya maskini, bali Bwana ndiye kimbilio lao.

7Laiti wokovu wa Israeli ungalikuja kutoka Sayuni! Wakati Bwana arejeshapo wafungwa wa watu wake, Yakobo na ashangilie, Israeli na afurahi!

Zaburi

Open the interactive reader to switch translations, adjust type, and mark verses — or browse verses by topic.

Neno: Bibilia Takatifu — Kiswahili Contemporary Version. Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. Used under the Biblica Open (Toleo Wazi) License. · Biblica Open License