Zaburi 138

Neno: Kiswahili Contemporary Version

1Nitakusifu wewe, Ee Bwana, kwa moyo wangu wote, mbele ya “miungu” nitaimba sifa zako.

2Nitasujudu nikielekea Hekalu lako takatifu, nami nitalisifu jina lako kwa ajili ya upendo wako na uaminifu, kwa kuwa umelikuza jina lako na neno lako juu ya vitu vyote.

3Nilipoita, ulinijibu; ulinifanya jasiri na mwenye moyo hodari.

4Wafalme wote wa dunia wakusifu wewe Ee Bwana, wakati wanaposikia maneno ya kinywa chako.

5Wao na waimbe kuhusu njia za Bwana, kwa maana utukufu wa Bwana ni mkuu.

6Ingawa Bwana yuko juu, humwangalia mnyonge, bali mwenye kiburi yeye anamjua kutokea mbali.

7Nijapopita katikati ya shida, wewe unayahifadhi maisha yangu, unanyoosha mkono wako dhidi ya hasira ya adui zangu, kwa mkono wako wa kuume unaniokoa.

8Bwana atatimiza kusudi lake kwangu, Ee Bwana, upendo wako wadumu milele: usiziache kazi za mikono yako.

Zaburi

Open the interactive reader to switch translations, adjust type, and mark verses — or browse verses by topic.

Neno: Bibilia Takatifu — Kiswahili Contemporary Version. Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. Used under the Biblica Open (Toleo Wazi) License. · Biblica Open License