Zaburi 147

Neno: Kiswahili Contemporary Version

1Msifuni Bwana. Tazama jinsi ilivyo vyema kumwimbia Mungu wetu sifa, jinsi inavyopendeza na kustahili kumsifu yeye!

2Bwana hujenga Yerusalemu, huwakusanya Israeli walio uhamishoni.

3Anawaponya waliovunjika mioyo na kuvifunga vidonda vyao.

4Huzihesabu nyota na huipa kila moja jina lake.

5Bwana wetu ni mkuu na mwenye uwezo mwingi, ufahamu wake hauna kikomo.

6Bwana huwahifadhi wanyenyekevu lakini huwashusha waovu mpaka mavumbini.

7Mwimbieni Bwana kwa shukrani, mpigieni Mungu wetu kinubi.

8Yeye huzifunika anga kwa mawingu, huinyeshea ardhi mvua, na kuzifanya nyasi kuota juu ya vilima.

9Huwapa chakula mifugo na pia makinda ya kunguru yanapolia.

10Furaha yake haipo katika nguvu za farasi, wala furaha yake kwenye miguu ya mwanadamu.

11Bwana hupendezwa na wale wamchao, wale wanaoweka tumaini lao katika upendo wake usiokoma.

12Mtukuze Bwana, ee Yerusalemu, msifu Mungu wako, ee Sayuni,

13kwa maana huimarisha makomeo ya malango yako na huwabariki watu wako walio ndani yako.

14Huwapa amani mipakani mwenu na kukushibisha kwa ngano safi kabisa.

15Hutuma amri yake duniani, neno lake hukimbia kasi.

16Anatandaza theluji kama sufu na kutawanya umande kama majivu.

17Huvurumisha mvua yake ya mawe kama changarawe. Ni nani awezaye kustahimili ukali wa baridi yake?

18Hutuma neno lake na kuviyeyusha, huvumisha upepo wake, nayo maji hutiririka.

19Amemfunulia Yakobo neno lake, sheria zake na maagizo yake kwa Israeli.

20Hajafanya hivyo kwa taifa lingine lolote, hawazijui sheria zake. Msifuni Bwana.

Zaburi

Open the interactive reader to switch translations, adjust type, and mark verses — or browse verses by topic.

Neno: Bibilia Takatifu — Kiswahili Contemporary Version. Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. Used under the Biblica Open (Toleo Wazi) License. · Biblica Open License