Zaburi 91

Neno: Kiswahili Contemporary Version

1Yeye akaaye mahali pa salama pake Yeye Aliye Juu Sana, atadumu katika uvuli wake Mwenyezi.

2Nitasema kumhusu Bwana, “Yeye ndiye kimbilio langu na ngome yangu, Mungu wangu, ambaye ninamtumaini.”

3Hakika yeye ataniokoa na mtego wa mwindaji, na maradhi ya kuambukiza ya kuua.

4Atakufunika kwa manyoya yake, chini ya mbawa zake utapata kimbilio, uaminifu wake utakuwa ngao na kinga yako.

5Hutaogopa vitisho vya usiku, wala mshale urukao mchana,

6wala maradhi ya kuambukiza yanayonyemelea gizani, wala tauni iharibuyo adhuhuri.

7Ijapo watu elfu wataangukia kando yako, kumi elfu mkono wako wa kuume, lakini haitakukaribia wewe.

8Utatazama tu kwa macho yako na kuona adhabu ya waovu.

9Kama ukimfanya Aliye Juu Sana kuwa makao yako: naam, Bwana ambaye ni kimbilio langu,

10basi hakuna madhara yatakayokupata wewe, hakuna maafa yataikaribia hema yako.

11Kwa kuwa atawaagiza malaika zake kwa ajili yako, wakulinde katika njia zako zote.

12Mikononi mwao watakuinua, ili usijikwae mguu wako kwenye jiwe.

13Utawakanyaga simba na nyoka wakali, simba mkubwa na nyoka utawaponda kwa miguu.

14Bwana asema, “Kwa kuwa ananipenda, nitamwokoa; nitamlinda, kwa kuwa analikiri Jina langu.

15Ataniita, nami nitamjibu; nitakuwa pamoja naye katika taabu, nitamwokoa na kumheshimu.

16Kwa siku nyingi nitamshibisha na kumwonyesha wokovu wangu.”

Zaburi

Open the interactive reader to switch translations, adjust type, and mark verses — or browse verses by topic.

Neno: Bibilia Takatifu — Kiswahili Contemporary Version. Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. Used under the Biblica Open (Toleo Wazi) License. · Biblica Open License