Zaburi 149

Neno: Kiswahili Contemporary Version

Msifuni Bwana. Mwimbieni Bwana wimbo mpya, sifa zake katika kusanyiko la watakatifu.

Israeli na washangilie katika Muumba wao, watu wa Sayuni na wafurahi katika Mfalme wao.

Na walisifu jina lake kwa kucheza na wampigie muziki kwa matari na kinubi.

Kwa maana Bwana anapendezwa na watu wake, anawavika wanyenyekevu taji ya wokovu.

Watakatifu washangilie katika heshima hii, na waimbe kwa shangwe vitandani mwao.

Sifa za Mungu na ziwe vinywani mwao na upanga ukatao kuwili mikononi mwao,

ili walipize mataifa kisasi na adhabu juu ya mataifa,

wawafunge wafalme wao kwa minyororo, wakuu wao kwa pingu za chuma,

ili kuwafanyia hukumu iliyoandikwa dhidi yao. Huu ndio utukufu wa watakatifu wake wote. Msifuni Bwana.

Zaburi

Fungua msomaji shirikishi ili kubadilisha tafsiri, kurekebisha herufi, na kutia alama mistari — au vinjari mistari kwa mada.

Neno: Bibilia Takatifu — Kiswahili Contemporary Version. Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. Used under the Biblica Open (Toleo Wazi) License. · Biblica Open License