Zaburi 92

Neno: Kiswahili Contemporary Version

1Ni vyema kumshukuru Bwana na kuliimbia jina lako, Ee Uliye Juu Sana,

2kuutangaza upendo wako asubuhi, na uaminifu wako wakati wa usiku,

3kwa zeze yenye nyuzi kumi na kwa sauti ya kinubi.

4Ee Bwana, kwa kuwa matendo yako yamenifurahisha, nitaziimba kwa shangwe kazi za mikono yako.

5Ee Bwana, tazama jinsi yalivyo makuu matendo yako, tazama jinsi yalivyo ya kina mawazo yako!

6Mjinga hafahamu, mpumbavu haelewi,

7ingawa waovu huchipua kama majani na wote watendao mabaya wanastawi, wataangamizwa milele.

8Bali wewe, Ee Bwana, utatukuzwa milele.

9Ee Bwana, hakika adui zako, hakika adui zako wataangamia. Wote watendao mabaya watatawanyika.

10Umeitukuza pembe yangu kama ile ya nyati dume, mafuta mazuri yamemiminwa juu yangu.

11Macho yangu yamewaona adui zangu wakishindwa, masikio yangu yamesikia maangamizi ya adui zangu waovu.

12Wenye haki watastawi kama mtende, watakuwa kama mwerezi wa Lebanoni,

13waliopandwa katika nyumba ya Bwana, watastawi katika nyua za Mungu wetu.

14Wakati wa uzee watakuwa bado wanazaa matunda, watakuwa wabichi tena wamejaa nguvu,

15wakitangaza, “ Bwana ni mkamilifu; yeye ni Mwamba wangu, na ndani yake hamna uovu.”

Zaburi

Open the interactive reader to switch translations, adjust type, and mark verses — or browse verses by topic.

Neno: Bibilia Takatifu — Kiswahili Contemporary Version. Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. Used under the Biblica Open (Toleo Wazi) License. · Biblica Open License