Zaburi 64

Neno: Kiswahili Contemporary Version

1Ee Mungu, unisikie ninapoeleza lalamiko langu, uyahifadhi maisha yangu kutokana na vitisho vya adui.

2Unifiche kutokana na shauri la siri la waovu, kutokana na zile kelele za kundi la watenda mabaya.

3Wananoa ndimi zao kama panga na kuelekeza maneno yao kama mishale ya kufisha.

4Hurusha mishale kutoka kwenye mavizio kwa mtu asiye na hatia, humrushia ghafula bila woga.

5Kila mmoja humtia moyo mwenzake katika mipango mibaya; huzungumza juu ya kuficha mitego yao, nao husema, “Ni nani ataiona?”

6Hufanya shauri baya la dhuluma na kusema, “Tumebuni mpango mkamilifu!” Hakika nia na moyo wa mwanadamu vina hila.

7Bali Mungu atawapiga kwa mishale, nao ghafula wataangushwa.

8Atageuza ndimi zao wenyewe dhidi yao na kuwaleta kwenye maangamizi; wote wawaonao watatikisa vichwa vyao kwa dharau.

9Wanadamu wote wataogopa, watatangaza kazi za Mungu na kutafakari yale aliyoyatenda.

10Wenye haki na wafurahi katika Bwana, na wakimbilie kwake; wanyofu wote wa moyo na wamsifu yeye!

Zaburi

Open the interactive reader to switch translations, adjust type, and mark verses — or browse verses by topic.

Neno: Bibilia Takatifu — Kiswahili Contemporary Version. Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. Used under the Biblica Open (Toleo Wazi) License. · Biblica Open License