Zaburi 98

Neno: Kiswahili Contemporary Version

1Mwimbieni Bwana wimbo mpya, kwa maana ametenda mambo ya ajabu; kitanga chake cha kuume na mkono wake mtakatifu umemfanyia wokovu.

2Bwana ameufanya wokovu wake ujulikane na amedhihirisha haki yake kwa mataifa.

3Ameukumbuka upendo wake na uaminifu wake kwa nyumba ya Israeli; miisho yote ya dunia imeuona wokovu wa Mungu wetu.

4Mpigieni Bwana kelele za shangwe, dunia yote, ipaze sauti kwa nyimbo za shangwe na vinanda;

5mwimbieni Bwana kwa kinubi, kwa kinubi na sauti za kuimba,

6kwa tarumbeta na mvumo wa baragumu za pembe za kondoo dume: shangilieni kwa furaha mbele za Bwana, aliye Mfalme.

7Bahari na ivume na kila kiliomo ndani yake, dunia na wote wakaao ndani yake.

8Mito na ipige makofi, milima na iimbe pamoja kwa furaha,

9vyote na viimbe mbele za Bwana, kwa maana yuaja kuhukumu dunia. Atahukumu dunia kwa haki na mataifa kwa haki.

Zaburi

Open the interactive reader to switch translations, adjust type, and mark verses — or browse verses by topic.

Neno: Bibilia Takatifu — Kiswahili Contemporary Version. Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. Used under the Biblica Open (Toleo Wazi) License. · Biblica Open License