Zaburi 26

Neno: Kiswahili Contemporary Version

1Ee Bwana, nithibitishe katika haki, maana nimeishi maisha yasiyo na lawama; nimemtumainia Bwana bila kusitasita.

2Ee Bwana, unijaribu, unipime, uuchunguze moyo wangu na mawazo yangu;

3kwa maana upendo wako uko mbele yangu daima, nami natembea siku zote katika kweli yako.

4Siketi pamoja na watu wadanganyifu, wala siandamani na wanafiki,

5ninachukia kusanyiko la watenda mabaya na ninakataa kuketi pamoja na waovu.

6Ninanawa mikono yangu kwa kuwa sina hatia, naikaribia madhabahu yako, Ee Bwana,

7nikitangaza sifa yako kwa sauti kubwa, huku nikisimulia matendo yako ya ajabu.

8Ee Bwana, naipenda nyumba yako mahali unakoishi, mahali ambapo utukufu wako hukaa.

9Usiiondoe nafsi yangu pamoja na watenda dhambi, wala uhai wangu pamoja na wamwagao damu,

10ambao mikononi mwao kuna mipango miovu, ambao mikono yao ya kuume imejaa rushwa.

11Bali mimi ninaishi maisha yasiyo na lawama; nikomboe na unihurumie.

12Miguu yangu imesimama katika uwanja tambarare; katika kusanyiko kuu nitamsifu Bwana.

Zaburi

Open the interactive reader to switch translations, adjust type, and mark verses — or browse verses by topic.

Neno: Bibilia Takatifu — Kiswahili Contemporary Version. Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. Used under the Biblica Open (Toleo Wazi) License. · Biblica Open License