Zaburi 28

Neno: Kiswahili Contemporary Version

1Ninakuita wewe, Ee Bwana, Mwamba wangu; usiwe kwangu kama kiziwi. Kwa sababu ukinyamaza nitafanana na walioshuka shimoni.

2Sikia kilio changu unihurumie ninapokuita kwa ajili ya msaada, niinuapo mikono yangu kuelekea Patakatifu pa Patakatifu pako.

3Usiniburute pamoja na waovu, pamoja na hao watendao mabaya, ambao huzungumza na jirani zao maneno mazuri, lakini mioyoni mwao wameficha chuki.

4Walipe sawasawa na matendo yao, sawasawa na matendo yao maovu; walipe sawasawa na kazi za mikono yao, uwalipe wanavyostahili.

5Kwa kuwa hawaheshimu kazi za Bwana, na yale ambayo mikono yake imetenda, atawabomoa na kamwe hatawajenga tena.

6Bwana asifiwe, kwa maana amesikia kilio changu nikimwomba anihurumie.

7Bwana ni nguvu zangu na ngao yangu, moyo wangu umemtumaini yeye, nami nimesaidiwa. Moyo wangu unarukaruka kwa furaha nami nitamshukuru kwa wimbo.

8Bwana ni nguvu ya watu wake, ngome ya wokovu kwa mpakwa mafuta wake.

9Waokoe watu wako na uubariki urithi wako; uwe mchungaji wao na uwabebe milele.

Zaburi

Open the interactive reader to switch translations, adjust type, and mark verses — or browse verses by topic.

Neno: Bibilia Takatifu — Kiswahili Contemporary Version. Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. Used under the Biblica Open (Toleo Wazi) License. · Biblica Open License