Zaburi 106

Neno: Kiswahili Contemporary Version

1Msifuni Bwana. Mshukuruni Bwana, kwa kuwa ni mwema; upendo wake wadumu milele.

2Ni nani awezaye kusimulia matendo makuu ya Bwana au kutangaza kikamilifu sifa zake?

3Heri wale wanaodumisha haki, ambao daima wanafanya yaliyo mema.

4Ee Bwana, unikumbuke unapowatendea mema watu wako, uwe msaada wangu unapowaokoa,

5ili niweze kufurahia mafanikio ya wateule wako, niweze kushiriki katika furaha ya taifa lako, na kuungana na urithi wako katika kukusifu.

6Tumetenda dhambi, kama vile baba zetu walivyotenda, tumekosa na tumetenda uovu.

7Wakati baba zetu walipokuwa Misri, hawakuzingatia maajabu yako, wala hawakukumbuka wingi wa fadhili zako, bali waliasi kando ya bahari, Bahari ya Shamu.

8Hata hivyo aliwaokoa kwa ajili ya jina lake, ili apate kudhihirisha uweza wake mkuu.

9Alikemea Bahari ya Shamu, nayo ikakauka, akawaongoza katika vilindi vyake kama vile jangwani.

10Aliwaokoa mikononi mwa adui; kutoka mikononi mwa adui aliwakomboa.

11Maji yaliwafunika adui zao, hakunusurika hata mmoja.

12Ndipo walipoamini ahadi zake, nao wakaimba sifa zake.

13Lakini mara walisahau aliyowatendea, wala hawakungojea shauri lake.

14Jangwani walitawaliwa na tamaa zao, walimjaribu Mungu nyikani.

15Kwa hiyo aliwapa kile walichoomba, lakini akatuma juu yao ugonjwa wa kudhoofisha.

16Kambini walimwonea wivu Mose, na pia Aroni aliyekuwa amewekwa wakfu kwa Bwana.

17Ardhi ilifunguka ikawameza Dathani, ikawazika Abiramu na kundi lake.

18Moto uliwaka katikati ya wafuasi wao, mwali wa moto uliwateketeza waovu.

19Huko Horebu walitengeneza ndama, na kuabudu sanamu ya kusubu kwa chuma.

20Waliubadilisha Utukufu wao kwa sanamu ya fahali, ambaye hula majani.

21Walimsahau Mungu aliyewaokoa, aliyekuwa ametenda mambo makuu huko Misri,

22miujiza katika nchi ya Hamu na mambo ya kutisha huko Bahari ya Shamu.

23Kwa hiyo alisema kwamba angewaangamiza: kama Mose mteule wake, asingesimama kati yao na Mungu kuizuia ghadhabu yake kuwaangamiza.

24Kisha waliidharau ile nchi nzuri, hawakuiamini ahadi yake.

25Walinungʼunika ndani ya mahema yao, wala hawakumtii Bwana.

26Kwa hiyo akaapa kwa mkono ulioinuliwa kwamba atawafanya waanguke jangwani,

27kuwatawanya wazao wao waanguke miongoni mwa mataifa, na kuwatawanya katika nchi zote.

28Walijifunga nira na Baali wa Peori, wakala dhabihu zilizotolewa kwa miungu isiyo na uhai.

29Waliichochea hasira ya Bwana, wakamkasirisha kwa matendo yao maovu, nayo tauni ikazuka katikati yao.

30Lakini Finehasi alisimama na kuingilia kati, nayo tauni ikazuiliwa.

31Hili likahesabiwa kwake haki, kwa vizazi visivyo na mwisho vijavyo.

32Kwenye maji ya Meriba, walimkasirisha Bwana, janga likampata Mose kwa sababu yao;

33kwa maana walimwasi Roho wa Mungu, na maneno yasiyofaa yakatoka midomoni kwa Mose.

34Hawakuyaangamiza yale mataifa kama Bwana alivyowaagiza,

35bali walijichanganya na mataifa na wakazikubali desturi zao.

36Waliabudu sanamu zao, zikawa mtego kwao.

37Wakawatoa wana wao na binti zao dhabihu kwa mashetani.

38Walimwaga damu isiyo na hatia, damu za wana wao na binti zao, ambao waliwatoa dhabihu kwa sanamu za Kanaani, nayo nchi ikanajisika kwa damu zao.

39Wakajinajisi wenyewe kwa yale waliyotenda; kwa matendo yao wenyewe wakajifanyia ukahaba.

40Kwa hiyo Bwana akawakasirikia watu wake na akauchukia sana urithi wake.

41Akawakabidhi kwa mataifa na adui zao wakawatawala.

42Adui zao wakawaonea na kuwatia chini ya mamlaka yao.

43Mara nyingi aliwaokoa lakini walikuwa wamezama kwenye uasi, nao wakajiharibu katika dhambi zao.

44Lakini akaangalia mateso yao wakati aliposikia kilio chao;

45kwa ajili yao akakumbuka agano lake, na kutokana na upendo wake mkuu akapooza hasira yake.

46Akawafanya wahurumiwe na wote waliowashikilia mateka.

47Ee Bwana Mungu wetu, tuokoe. Tukusanye tena kutoka kwa mataifa, ili tuweze kulishukuru jina lako takatifu, na kushangilia katika sifa zako.

48Atukuzwe Bwana, Mungu wa Israeli, tangu milele na hata milele. Watu wote na waseme, “Amen!” Msifuni Bwana.

Zaburi

Open the interactive reader to switch translations, adjust type, and mark verses — or browse verses by topic.

Neno: Bibilia Takatifu — Kiswahili Contemporary Version. Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. Used under the Biblica Open (Toleo Wazi) License. · Biblica Open License