Zaburi 66

Neno: Kiswahili Contemporary Version

1Mpigieni Mungu kelele za shangwe, dunia yote!

2Imbeni utukufu wa jina lake; mpeni sifa zake kwa utukufu!

3Mwambieni Mungu, “Jinsi gani yalivyo ya kutisha matendo yako! Uwezo wako ni mkuu mno kiasi kwamba adui wananyenyekea mbele zako.

4Dunia yote yakusujudia, wanakuimbia wewe sifa, wanaliimbia sifa jina lako.”

5Njooni mwone yale Mungu aliyoyatenda, mambo ya kutisha aliyoyatenda miongoni mwa wanadamu!

6Alifanya bahari kuwa nchi kavu, wakapita kati ya maji kwa miguu, njooni, tumshangilie.

7Yeye hutawala kwa uwezo wake milele, macho yake huangalia mataifa yote: waasi wasithubutu kujiinua dhidi yake.

8Enyi mataifa, msifuni Mungu wetu, sauti ya sifa yake isikike,

9ameyahifadhi maisha yetu na kuizuia miguu yetu kuteleza.

10Ee Mungu, wewe ulitujaribu, ukatusafisha kama fedha.

11Umetuingiza kwenye nyavu na umetubebesha mizigo mizito migongoni mwetu.

12Uliwaruhusu watu watukalie vichwani, tulipita kwenye moto na kwenye maji, lakini ulituleta kwenye nchi iliyojaa utajiri tele.

13Nitakuja hekaluni mwako na sadaka za kuteketezwa na kukutimizia nadhiri zangu:

14nadhiri ambazo midomo yangu iliahidi na nilizotamka kwa kinywa changu nilipokuwa katika shida.

15Nitakutolea dhabihu za wanyama wanono na sadaka za kondoo dume, nitakutolea mafahali na mbuzi.

16Njooni msikilize ninyi nyote mnaomcha Mungu, nami niwaambie aliyonitendea.

17Nilimlilia kwa kinywa changu, sifa zake zilikuwa katika ulimi wangu.

18Kama ningekuwa nimeyaficha maovu moyoni mwangu, Bwana asingekuwa amenisikiliza;

19lakini hakika Mungu amenisikiliza na amesikia sauti yangu katika maombi.

20Sifa apewe Mungu, ambaye hakulikataa ombi langu wala kunizuilia upendo wake!

Zaburi

Open the interactive reader to switch translations, adjust type, and mark verses — or browse verses by topic.

Neno: Bibilia Takatifu — Kiswahili Contemporary Version. Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. Used under the Biblica Open (Toleo Wazi) License. · Biblica Open License