Zaburi 141

Neno: Kiswahili Contemporary Version

Ee Bwana, ninakuita wewe, uje kwangu hima. Sikia sauti yangu ninapokuita.

Maombi yangu na yafike mbele zako kama uvumba; kuinua mikono yangu juu na kuwe kama dhabihu ya jioni.

Ee Bwana, weka mlinzi kinywani mwangu, weka ulinzi mlangoni mwa midomo yangu.

Usiuache moyo wangu uvutwe katika jambo baya, nisije nikashiriki katika matendo maovu pamoja na watu watendao mabaya, wala nisije nikala vyakula vyao vya anasa.

Mtu mwenye haki na anipige: ni jambo la huruma; na anikemee: ni mafuta kichwani mwangu. Kichwa changu hakitalikataa. Hata hivyo, maombi yangu daima ni kinyume cha watenda mabaya,

watawala wao watatupwa chini kutoka kwenye majabali, waovu watajifunza kwamba maneno yangu yalikuwa kweli.

Watasema, “Kama mtu anavyolima na kuvunja ardhi, ndivyo mifupa yetu imetawanywa kwenye mlango wa kaburi.”

Lakini nimekaza macho yangu kwako, Ee Bwana Mwenyezi, ndani yako nimekimbilia, usiniache nife.

Niepushe na mitego waliyonitegea, kutokana na mitego iliyotegwa na watenda mabaya.

Waovu na waanguke kwenye nyavu zao wenyewe, wakati mimi ninapita salama.

Zaburi

Fungua msomaji shirikishi ili kubadilisha tafsiri, kurekebisha herufi, na kutia alama mistari — au vinjari mistari kwa mada.

Neno: Bibilia Takatifu — Kiswahili Contemporary Version. Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. Used under the Biblica Open (Toleo Wazi) License. · Biblica Open License