Zaburi 35

Neno: Kiswahili Contemporary Version

1Ee Bwana, pingana na wale wanaopingana nami, upigane na hao wanaopigana nami.

2Chukua ngao na kigao. Inuka unisaidie.

3Inua mkuki wako na fumo lako dhidi ya hao wanaonifuatia. Iambie nafsi yangu, “Mimi ni wokovu wako.”

4Wafedheheshwe na waaibishwe wale wanaotafuta uhai wangu. Wanaofanya shauri kuniangamiza warudishwe nyuma kwa hofu.

5Wawe kama makapi yapeperushwayo na upepo, malaika wa Bwana akiwafukuza.

6Njia yao na iwe giza na ya utelezi, malaika wa Bwana akiwafuatilia.

7Kwa vile walinifichia wavu wao bila sababu, na bila sababu wamenichimbia shimo,

8maafa na yawapate ghafula: wavu walionifichia na uwatege wenyewe, na waanguke katika shimo hilo, kwa maangamizo yao.

9Ndipo nafsi yangu itashangilia katika Bwana na kuufurahia wokovu wake.

10Nitapaza sauti yangu nikisema, “Ni nani aliye kama wewe, Ee Bwana? Wewe huwaokoa maskini kutokana na wale walio na nguvu kuliko wao, maskini na mhitaji kutokana na wanaowanyangʼanya!”

11Mashahidi wakatili wanainuka, wananiuliza mambo nisiyoyajua.

12Wananilipa baya kwa jema na kuiacha nafsi yangu ukiwa.

13Lakini walipokuwa wagonjwa, nilivaa nguo ya gunia na nikajinyenyekesha kwa kufunga. Maombi yangu yaliponirudia bila kujibiwa,

14niliendelea kuomboleza kama vile wao ni rafiki au ndugu. Niliinamisha kichwa chini kwa huzuni kama ninayemwombolezea mama yangu.

15Lakini nilipojikwaa, walikusanyika kwa shangwe; washambuliaji walijikusanya dhidi yangu bila mimi kujua. Walinisingizia pasipo kukoma.

16Kama watu wasiomcha Mungu, wamenidhihaki, wamenisagia meno.

17Ee Bwana, utatazama mpaka lini? Niokoe maisha yangu na maangamizi yao, uhai wangu wa thamani kutokana na simba hawa.

18Nami nitakushukuru mbele ya kusanyiko kubwa, nitakusifu katikati ya watu wengi.

19Usiwaache wale wanaonisimanga, wale ambao ni adui zangu bila sababu; usiwaache wale ambao ni adui zangu bila sababu wakonyeze jicho kwa hila.

20Hawazungumzi kwa amani, bali wanatunga mashtaka ya uongo dhidi ya wale wanaoishi kwa utulivu katika nchi.

21Hunifumbulia vinywa vyao wakisema, “Aha! Aha! Kwa macho yetu wenyewe tumeliona.”

22Ee Bwana, umeona hili, usiwe kimya. Usiwe mbali nami, Ee Bwana.

23Amka, inuka unitetee! Unipiganie Mungu wangu na Bwana wangu.

24Nihukumu kwa haki yako, Ee Bwana Mungu wangu, sawasawa na haki yako; usiwaache wakusimange.

25Usiwaache wafikiri, “Aha, hili ndilo tulilotaka!” Au waseme, “Tumemmeza.”

26Wote wanaofurahia dhiki yangu waaibishwe na wachanganyikiwe; hao wanaojiinua dhidi yangu wavikwe aibu na dharau.

27Wale wanaofurahia hukumu yangu ya haki wapige kelele za shangwe na furaha; hebu waseme siku zote, “ Bwana atukuzwe, ambaye amefurahia mafanikio ya mtumishi wake.”

28Ulimi wangu utanena haki yako na sifa zako mchana kutwa.

Zaburi

Open the interactive reader to switch translations, adjust type, and mark verses — or browse verses by topic.

Neno: Bibilia Takatifu — Kiswahili Contemporary Version. Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. Used under the Biblica Open (Toleo Wazi) License. · Biblica Open License