Zaburi 118

Neno: Kiswahili Contemporary Version

1Mshukuruni Bwana, kwa kuwa ni mwema; upendo wake wadumu milele.

2Israeli na aseme sasa: “Upendo wake wadumu milele.”

3Nyumba ya Aroni na iseme sasa: “Upendo wake wadumu milele.”

4Wote wamchao Bwana na waseme sasa: “Upendo wake wadumu milele.”

5Wakati wa maumivu yangu makuu nilimlilia Bwana, naye akanijibu kwa kuniweka huru.

6Bwana yuko pamoja nami, sitaogopa. Mwanadamu anaweza kunitenda nini?

7Bwana yuko pamoja nami, yeye ni msaidizi wangu. Nitawatazama adui zangu wakiwa wameshindwa.

8Ni bora kumkimbilia Bwana kuliko kumtumainia mwanadamu.

9Ni bora kumkimbilia Bwana kuliko kuwatumainia wakuu.

10Mataifa yote yalinizunguka, lakini kwa jina la Bwana naliwakatilia mbali.

11Walinizunguka pande zote, lakini kwa jina la Bwana naliwakatilia mbali.

12Walinizunguka kama kundi la nyuki, lakini walikufa haraka kama miiba iteketeayo; kwa jina la Bwana naliwakatilia mbali.

13Nilisukumwa nyuma karibu kuanguka, lakini Bwana alinisaidia.

14Bwana ni nguvu yangu na wimbo wangu, yeye amefanyika wokovu wangu.

15Sauti za shangwe na ushindi zinavuma hemani mwa wenye haki: “Mkono wa kuume wa Bwana umetenda mambo makuu!

16Mkono wa kuume wa Bwana umeinuliwa juu, mkono wa kuume wa Bwana umetenda mambo makuu!”

17Sitakufa, bali nitaishi, nami nitatangaza yale Bwana aliyoyatenda.

18Bwana ameniadhibu vikali, lakini hakuniacha nife.

19Nifungulie malango ya haki, nami nitaingia na kumshukuru Bwana.

20Hili ni lango la Bwana ambalo wenye haki wanaweza kuliingia.

21Nitakushukuru, kwa kuwa ulinijibu, umekuwa wokovu wangu.

22Jiwe walilolikataa waashi, limekuwa jiwe kuu la pembeni.

23Bwana ametenda hili, nalo ni la kushangaza machoni petu.

24Hii ndiyo siku Bwana aliyoifanya, tushangilie na kufurahi ndani yake.

25Ee Bwana, tuokoe, Ee Bwana, utujalie mafanikio.

26Heri yule ajaye kwa jina la Bwana. Kutoka nyumba ya Bwana tunakubariki.

27Bwana ndiye Mungu, naye ametuangazia nuru yake. Mkiwa na matawi mkononi, unganeni kwenye maandamano ya sikukuu hadi kwenye pembe za madhabahu.

28Wewe ni Mungu wangu, nitakushukuru, wewe ni Mungu wangu, nitakutukuza.

29Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema; upendo wake wadumu milele.

Zaburi

Open the interactive reader to switch translations, adjust type, and mark verses — or browse verses by topic.

Neno: Bibilia Takatifu — Kiswahili Contemporary Version. Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. Used under the Biblica Open (Toleo Wazi) License. · Biblica Open License