Zaburi 25

Neno: Kiswahili Contemporary Version

1Kwako wewe, Ee Bwana, nainua nafsi yangu,

2ni wewe ninayekutumainia, Ee Mungu wangu. Usiniache niaibike, wala usiache adui zangu wakanishinda.

3Kamwe hakuna hata mmoja anayekutegemea atakayeaibishwa, bali wataaibishwa wafanyao hila bila sababu.

4Nionyeshe njia zako, Ee Bwana, nifundishe mapito yako,

5niongoze katika kweli yako na kunifundisha, kwa maana wewe ni Mungu Mwokozi wangu, nalo tumaini langu liko kwako wakati wote.

6Kumbuka, Ee Bwana, rehema zako kuu na upendo, kwa maana zimekuwepo tangu zamani.

7Usizikumbuke dhambi za ujana wangu wala njia zangu za uasi, sawasawa na upendo wako unikumbuke, kwa maana wewe ni mwema, Ee Bwana.

8Bwana ni mwema na mwenye adili, kwa hiyo huwafundisha wenye dhambi njia zake.

9Huwaongoza wanyenyekevu katika haki, naye huwafundisha njia yake.

10Njia zote za Bwana ni za upendo na uaminifu kwa wale wanaoshika shuhuda za agano lake.

11Ee Bwana, kwa ajili ya jina lako, unisamehe uovu wangu, ijapokuwa ni mwingi.

12Ni nani basi, mtu yule anayemcha Bwana? Atamfundisha katika njia atakayoichagua kwa ajili yake.

13Mtu huyo atafanikiwa maishani mwake, nao wazao wake watairithi nchi.

14Siri ya Bwana iko kwa wale wamchao, yeye huwajulisha agano lake.

15Macho yangu humwelekea Bwana daima, kwa kuwa yeye peke yake ndiye ataitoa miguu yangu kutoka mtego.

16Nigeukie na unihurumie, kwa maana mimi ni mpweke na mwenye kuteseka.

17Shida za moyo wangu zimeongezeka, niokoe katika dhiki yangu.

18Uangalie mateso na shida zangu na uniondolee dhambi zangu zote.

19Tazama adui zangu walivyo wengi, pia uone jinsi wanavyonichukia vikali!

20Uyalinde maisha yangu na uniokoe, usiniache niaibike, kwa maana nimekukimbilia wewe.

21Uadilifu na uaminifu vinilinde, kwa sababu tumaini langu ni kwako.

22Ee Mungu, wakomboe Israeli, katika shida zao zote!

Zaburi

Open the interactive reader to switch translations, adjust type, and mark verses — or browse verses by topic.

Neno: Bibilia Takatifu — Kiswahili Contemporary Version. Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. Used under the Biblica Open (Toleo Wazi) License. · Biblica Open License