Zaburi 76

Open Word Bible

Mungu amejitambulisha katika Yuda; jina lake limetukuka katika Israeli. Makao yake yamewekwa Salemu, pango lake katika Sayuni. Huko alivunjavunja mishale ya moto ya upinde, ngao na upanga na zana zote za vita. Sela Wewe unang’aa kwa nuru, kwa fahari kuliko milima ya mawindo. Mashujaa wamenyang’anywa kila kitu; wamelala usingizi wao wa mwisho, wala hakuna hata mmoja wa wapiganaji aliyeweza kuinua mkono. Wewe ulipowakemea, Ee Mungu wa Yakobo, gari la vita na farasi walizimia. Wewe, naam, wewe ndiwe wa kuogopwa! Hasira yako inapowaka, ni nani awezaye kusimama mbele yako? Kutoka mbinguni wewe ulitangaza hukumu yako; dunia iliogopa ikanyamaza, Mungu aliposimama kutoa hukumu na kuwaokoa wanyonge wote duniani. Sela Hata ghadhabu ya wanadamu itaishia katika kukusifu wewe; kile kinachobaki wewe utakifunga kama mshipi. Mwekeeni BWANA Mungu wenu nadhiri, mkazitimize; wote wanaomzunguka na wamletee kodi Yeye aletaye hofu. Hukatiza pumzi ya wakuu; wafalme wa dunia humwogopa yeye.

Zaburi

Fungua msomaji shirikishi ili kubadilisha tafsiri, kurekebisha herufi, na kutia alama mistari — au vinjari mistari kwa mada.

Manukuu ya Maandiko yametoka katika Open Word Bible, ambayo iko katika uwanja wa umma.