Zaburi 57

Neno: Kiswahili Contemporary Version

Unihurumie, Ee Mungu, unihurumie, kwa maana nafsi yangu inakukimbilia. Chini ya uvuli wa mbawa zako nitakimbilia mpaka maafa yapite.

Namlilia Mungu Aliye Juu Sana, Mungu atimizaye makusudi yake kwangu.

Hutumana kutoka mbinguni na kuniokoa, akiwakemea wale wanaonifuatilia vikali; Mungu huutuma upendo wake na uaminifu wake.

Niko katikati ya simba, nimelala katikati ya wanyama wenye njaa kuu: watu ambao meno yao ni mikuki na mishale, ambao ndimi zao ni panga kali.

Ee Mungu, utukuzwe juu ya mbingu, utukufu wako na uenee duniani kote.

Waliitegea miguu yangu nyavu, nikainamishwa chini na dhiki. Wamechimba shimo katika njia yangu, lakini wametumbukia humo wao wenyewe.

Ee Mungu, moyo wangu ni thabiti; nitaimba na kusifu kwa moyo wangu wote.

Amka, nafsi yangu! Amka, kinubi na zeze! Nitayaamsha mapambazuko.

Nitakusifu wewe, Ee Bwana, katikati ya mataifa; nitaimba habari zako, katikati ya jamaa za watu.

Kwa maana upendo wako ni mkuu, waenea hadi mbinguni, uaminifu wako unazifikia anga.

Ee Mungu, utukuzwe juu mbinguni, utukufu wako na uwe duniani pote.

Zaburi

Fungua msomaji shirikishi ili kubadilisha tafsiri, kurekebisha herufi, na kutia alama mistari — au vinjari mistari kwa mada.

Neno: Bibilia Takatifu — Kiswahili Contemporary Version. Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. Used under the Biblica Open (Toleo Wazi) License. · Biblica Open License