Zaburi 21

Neno: Kiswahili Contemporary Version

1Ee Bwana, mfalme huzifurahia nguvu zako. Tazama jinsi ilivyo kuu furaha yake kwa ushindi unaompa!

2Umempa haja ya moyo wake na hukumzuilia maombi ya midomo yake.

3Ulimkaribisha kwa baraka tele na kumvika taji ya dhahabu safi kichwani pake.

4Alikuomba maisha, nawe ukampa, wingi wa siku milele na milele.

5Kutokana na ushindi uliompa, utukufu wake ni mkubwa, umeweka juu yake fahari na utukufu.

6Hakika umempa baraka za milele, umemfanya awe na furaha kwa shangwe ya uwepo wako.

7Kwa kuwa mfalme anamtumaini Bwana; kwa upendo usiokoma wa Aliye Juu Sana hatatikiswa.

8Mkono wako utawashika adui zako wote, mkono wako wa kuume utawakamata adui zako.

9Wakati utakapojitokeza utawafanya kama tanuru ya moto. Katika ghadhabu yake Bwana atawameza, moto wake utawateketeza.

10Utawaangamiza wazao wao kutoka duniani, uzao wao kutoka wanadamu.

11Ingawa watapanga mabaya dhidi yako na kutunga hila, hawawezi kufanikiwa,

12kwa kuwa utawafanya wakimbie utakapowalenga usoni pao kwa mshale kutoka kwenye upinde wako.

13Ee Bwana, utukuzwe katika nguvu zako, tutaimba na kusifu nguvu zako.

Zaburi

Open the interactive reader to switch translations, adjust type, and mark verses — or browse verses by topic.

Neno: Bibilia Takatifu — Kiswahili Contemporary Version. Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. Used under the Biblica Open (Toleo Wazi) License. · Biblica Open License