Zaburi 41

Neno: Kiswahili Contemporary Version

Heri mtu yule anayemjali mnyonge, Bwana atamwokoa wakati wa shida.

Bwana atamlinda na kuyahifadhi maisha yake, atambariki katika nchi na hatamwacha katika tamaa ya adui zake.

Bwana atamtegemeza awapo mgonjwa kitandani, atamwinua kutoka kitandani mwake.

Nilisema, “Ee Bwana nihurumie, niponye, maana nimekutenda dhambi wewe.”

Adui zangu wanasema kwa hila, “Lini atakufa, na jina lake litokomee kabisa.”

Kila anapokuja mtu kunitazama, huzungumza uongo, huku moyo wake hukusanya masingizio; kisha huondoka na kuyasambaza huku na huko.

Adui zangu wote hunongʼonezana dhidi yangu, hao huniwazia mabaya sana, wakisema,

“Ugonjwa mbaya sana umempata, kamwe hatainuka tena kitandani mwake.”

Hata rafiki yangu wa karibu niliyemwamini, yule aliyekula chakula changu ameniinulia kisigino chake.

Lakini wewe, Ee Bwana, nihurumie, ukaniinue tena, ili niweze kuwalipiza kisasi.

Najua kwamba wapendezwa nami, kwa kuwa adui yangu hanishindi.

Katika uadilifu wangu unanitegemeza na kuniweka kwenye uwepo wako milele.

Msifuni Bwana, Mungu wa Israeli, tangu milele na hata milele. Amen na Amen.

Zaburi

Fungua msomaji shirikishi ili kubadilisha tafsiri, kurekebisha herufi, na kutia alama mistari — au vinjari mistari kwa mada.

Neno: Bibilia Takatifu — Kiswahili Contemporary Version. Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. Used under the Biblica Open (Toleo Wazi) License. · Biblica Open License