Mithali 25

Neno: Kiswahili Contemporary Version

1Hizi ni mithali zaidi za Solomoni, zilizonakiliwa na watu wa Hezekia mfalme wa Yuda:

2Ni Utukufu wa Mungu kuficha jambo, bali ni utukufu wa wafalme kuchunguza jambo.

3Kama mbingu zilivyo juu na nchi ilivyo chini, ndivyo ambavyo mioyo ya wafalme haichunguziki.

4Ondoa takataka kwenye madini ya fedha, nako ndani yake kutatokea chombo cha mfua fedha.

5Ondoa waovu mbele ya mfalme, nacho kiti chake cha enzi kitaimarishwa kwa njia ya haki.

6Usijikweze mwenyewe mbele ya mfalme, wala usidai nafasi miongoni mwa watu wakuu;

7ni afadhali yeye akuambie, “Njoo huku juu,” kuliko yeye kukuaibisha mbele ya mkuu. Kile ulichokiona kwa macho yako

8usiharakishe kukipeleka mahakamani, maana utafanya nini mwishoni kama jirani yako atakuaibisha?

9Kama ukifanya shauri na jirani yako, usisaliti siri ya mtu mwingine,

10ama yeye aisikiaye aweza kukuaibisha na kamwe sifa yako mbaya haitaondoka.

11Neno lisemwalo kwa wakati ufaao ni kama matunda ya mtofaa ya dhahabu yaliyowekwa kwenye vijalizo vya fedha.

12Kama vile kipuli cha dhahabu au pambo la dhahabu safi, ndivyo lilivyo karipio la mtu mwenye hekima kwa sikio lisikilizalo.

13Kama vile ubaridi wa theluji wakati wa mavuno ndivyo alivyo mjumbe mwaminifu kwa wale wamtumao, huburudisha roho za bwana zake.

14Kama vile mawingu na upepo pasipo mvua ndivyo alivyo mtu ajisifuye kwa zawadi ambazo hatoi.

15Kwa njia ya uvumilivu mtawala aweza kushawishiwa, nao ulimi laini waweza kuvunja mfupa.

16Ukipata asali, kula kiasi tu cha kukutosha, ukila zaidi, utatapika.

17Ingiza mguu wako nyumbani kwa jirani yako mara chache, ukizidisha, atakukinai na atakuchukia.

18Kama vile rungu au upanga au mshale mkali ndivyo alivyo mtu atoaye ushuhuda wa uongo dhidi ya jirani yake.

19Kama vile jino bovu au mguu uliolemaa, ndivyo ilivyo kumtegemea mtu asiye mwaminifu wakati wa shida.

20Kama vile avuaye mavazi siku ya baridi, au kama siki iliyomwagwa juu ya magadi, ndivyo alivyo yeye amuimbiaye nyimbo mtu mwenye moyo mzito.

21Kama adui yako ana njaa, mpe chakula ale; kama ana kiu, mpe maji anywe.

22Kwa kufanya hivyo, unaweka makaa ya moto yanayowaka kichwani pake, naye Bwana atakupa thawabu.

23Kama vile upepo wa kaskazini uletavyo mvua, ndivyo ulimi usingiziao uletavyo uso wa hasira.

24Ni afadhali kuishi pembeni mwa paa la nyumba, kuliko kuishi nyumba moja na mke mgomvi.

25Kama vile maji baridi kwa nafsi iliyochoka ndivyo zilivyo habari njema kutoka nchi ya mbali.

26Kama vile chemchemi iliyotibuliwa matope au kisima kilichotiwa taka ndivyo alivyo mtu mwenye haki akishiriki na waovu.

27Si vyema kula asali nyingi sana, wala si heshima kujitafutia heshima yako mwenyewe.

28Kama vile mji ambao kuta zake zimebomoka ndivyo alivyo mtu ambaye hawezi kujitawala mwenyewe.

Mithali

Open the interactive reader to switch translations, adjust type, and mark verses — or browse verses by topic.

Neno: Bibilia Takatifu — Kiswahili Contemporary Version. Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. Used under the Biblica Open (Toleo Wazi) License. · Biblica Open License