Mithali 17
Neno: Kiswahili Contemporary Version
1Afadhali kula ukoko mkavu ukiwa na amani na utulivu kuliko kukaa kwenye nyumba ya karamu kukiwa na magomvi.
2Mtumishi mwenye hekima atatawala juu ya mwana aaibishaye, naye atashirikiana katika urithi kama mmoja wa hao ndugu.
3Kalibu ni kwa ajili ya fedha na tanuru ni kwa ajili ya dhahabu, bali Bwana huujaribu moyo.
4Mtu mwovu husikiliza midomo mibaya; mwongo husikiliza kwa makini ulimi wa madhara.
5Yeye anaye mdhihaki maskini huonyesha dharau kwa Muumba wake; yeyote afurahiaye maafa hataepuka kuadhibiwa.
6Wana wa wana ni taji la wazee, nao wazazi ni fahari ya watoto wao.
7Midomo yenye uwezo wa ushawishi haimfai mpumbavu: je, ni mibaya kiasi gani zaidi midomo ya uongo kwa mtawala!
8Kipawa ni kama kito cha thamani machoni pake yeye aliye nacho; kokote kigeukiapo, hufanikiwa.
9Yeye anayesamehe kosa hudumisha upendo, bali yeyote arudiaye jambo hutenganisha marafiki wa karibu.
10Karipio humwingia sana mtu mwenye kutambua kuliko mapigo mia kwa mpumbavu.
11Mtu mbaya hupenda kuasi tu; mjumbe asiye na huruma atatumwa dhidi yake.
12Ni afadhali ukutane na dubu aliyenyangʼanywa watoto wake, kuliko mpumbavu katika upumbavu wake.
13Ikiwa mtu atalipa baya kwa jema, kamwe ubaya hautaondoka katika nyumba yake.
14Kuanzisha ugomvi ni kama kutoboa bwawa la maji; kwa hiyo acha jambo hilo kabla mabishano hayajaanza.
15Yeye asemaye kuwa asiye na haki ana haki, naye asemaye kuwa mwenye haki hana haki: Bwana huwachukia sana wote wawili.
16Fedha ina faida gani mikononi mwa mpumbavu, wakati yeye hana haja ya kupata hekima?
17Rafiki hupenda wakati wote naye ndugu amezaliwa kwa ajili ya wakati wa shida.
18Mtu mjinga hupana mkono ili kuweka rehani, naye huweka dhamana kwa jirani yake.
19Yeye apendaye ugomvi apenda dhambi; naye ainuaye sana lango lake hutafuta uharibifu.
20Mtu mwenye moyo mpotovu hawezi kufanikiwa; naye ambaye ulimi wake ni mdanganyifu huanguka kwenye taabu.
21Kuwa na mwana mpumbavu huleta huzuni; hakuna furaha kwa baba wa mpumbavu.
22Moyo wenye furaha ni dawa nzuri, bali roho iliyopondeka hukausha mifupa.
23Mtu mwovu hukubali rushwa kwa siri ili kupotosha njia ya haki.
24Mtu wa ufahamu huitazama hekima, lakini macho ya mpumbavu huhangaika hadi kwenye miisho ya dunia.
25Mwana mpumbavu huleta huzuni kwa baba yake na uchungu kwa yeye aliyemzaa.
26Si vizuri kumwadhibu mtu asiye na hatia, au kuwapiga sana maafisa kwa ajili ya uadilifu wao.
27Mtu mwenye maarifa hutumia maneno kwa kujizuia, naye mtu mwenye ufahamu ana moyo wa utulivu.
28Hata mtu mpumbavu hudhaniwa kuwa na hekima kama akinyamaza, na mwenye ufahamu kama akiuzuia ulimi wake.
Mithali
Open the interactive reader to switch translations, adjust type, and mark verses — or browse verses by topic.
Neno: Bibilia Takatifu — Kiswahili Contemporary Version. Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. Used under the Biblica Open (Toleo Wazi) License. · Biblica Open License