Mithali 2
Neno: Kiswahili Contemporary Version
1Mwanangu, kama utayakubali maneno yangu na kuyaweka akiba maagizo yangu ndani mwako,
2kutega sikio lako kwenye hekima na kuweka moyo wako katika ufahamu,
3na kama ukiita busara na kuita kwa sauti ufahamu,
4na kama utaitafuta kama fedha na kuitafuta sana kama hazina iliyofichwa,
5ndipo utakapoelewa kumcha Bwana na kupata maarifa ya Mungu.
6Kwa maana Bwana hutoa hekima, na kinywani mwake hutoka maarifa na ufahamu.
7Anahifadhi ushindi kwa ajili ya mwadilifu, yeye ni ngao kwa wale wasio na lawama,
8kwa kuwa hulinda mwenendo wa mwenye haki na kuhifadhi njia ya waaminifu wake.
9Ndipo utafahamu lipi lililo kweli na haki na sawa: yaani kila njia nzuri.
10Kwa maana hekima itaingia moyoni mwako, nayo maarifa yataifurahisha nafsi yako.
11Busara itakuhifadhi na ufahamu utakulinda.
12Hekima itakuokoa kutoka njia za waovu, kutoka kwa watu ambao maneno yao yamepotoka,
13wale waachao mapito yaliyonyooka wakatembea katika njia za giza,
14wale wapendao kutenda mabaya na kufurahia upotovu wa ubaya,
15ambao mapito yao yamepotoka na ambao ni wapotovu katika njia zao.
16Itakuokoa pia kutokana na mwanamke kahaba, kutokana na mke aliyepotoka mwenye maneno ya kushawishi kutenda ubaya,
17aliyemwacha mwenzi wa ujana wake na kupuuza agano alilofanya mbele ya Mungu.
18Kwa maana nyumba yake huelekea kwenye kifo na mapito yake kwenye roho za waliokufa.
19Hakuna yeyote aendaye kwake akarudi, au kufikia mapito ya uzima.
20Hivyo utatembea katika njia za watu wema na kushikamana na mapito ya wenye haki.
21Kwa maana wanyofu wataishi katika nchi, nao wasio na lawama watabakia ndani yake.
22Bali waovu watakatiliwa mbali kutoka nchi, nao wasio waaminifu watangʼolewa kutoka humo.
Mithali
Open the interactive reader to switch translations, adjust type, and mark verses — or browse verses by topic.
Neno: Bibilia Takatifu — Kiswahili Contemporary Version. Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. Used under the Biblica Open (Toleo Wazi) License. · Biblica Open License