1 Mambo ya Nyakati 18

Open Word Bible

Baada ya hayo, Daudi aliwashinda Wafilisti akawaweka chini ya mamlaka yake. Akautwaa Gathi na vijiji vyake kutoka mikononi mwa Wafilisti. Aliwashinda pia Moabu, nao Wamoabu wakawa chini ya Daudi, wakamletea kodi. Daudi alimshinda pia Hadadezeri mfalme wa Soba, kuelekea Hamathi, Hadadezeri alipokwenda kusimamisha mnara wake wa ukumbusho kwenye mto Frati. Daudi aliteka kwake magari ya vita 1,000, wapanda farasi 7,000 na askari wa miguu 20,000. Akawakata mishipa ya miguu farasi wote wa magari ya vita, lakini akabakiza wa kutosha magari mia moja. Waaramu wa Dameski walipokuja kumsaidia Hadadezeri mfalme wa Soba, Daudi aliwaua Waaramu 22,000. Kisha Daudi akaweka vikosi vya askari katika Aramu wa Dameski. Waaramu wakawa chini ya Daudi, wakamletea kodi. BWANA alimpa Daudi ushindi kila alikokwenda. Daudi alichukua ngao za dhahabu walizokuwa wamebeba maafisa wa Hadadezeri, akazileta Yerusalemu. Kutoka Tibhathi na Kuni, miji ya Hadadezeri, Daudi alichukua shaba nyingi sana. Kwa shaba hiyo Sulemani aliifanya Bahari ya shaba, nguzo na vyombo vya shaba.

Tou mfalme wa Hamathi aliposikia kwamba Daudi amelishinda jeshi lote la Hadadezeri mfalme wa Soba, alimtuma mwanawe Hadoramu kwa mfalme Daudi kumsalimu na kumpongeza kwa kupigana na Hadadezeri na kumshinda, kwa maana Hadadezeri na Tou walikuwa wamepigana vita mara nyingi. Hadoramu alileta kila aina ya vyombo vya dhahabu, fedha na shaba. Mfalme Daudi alimwekea BWANA wakfu vitu hivyo pia, kama alivyofanya kwa fedha na dhahabu aliyochukua kutoka mataifa yote: kutoka Edomu, Moabu, Waamoni, Wafilisti na Amaleki. Abishai mwana wa Seruya aliwaua Waedomu 18,000 katika Bonde la Chumvi. Aliweka vikosi vya askari katika Edomu, na Waedomu wote wakawa chini ya Daudi. BWANA alimpa Daudi ushindi kila alikokwenda. Basi Daudi alitawala juu ya Israeli wote, naye akawatendea watu wake wote yaliyo ya haki na ya adili. Yoabu mwana wa Seruya alikuwa mkuu wa jeshi; Yehoshafati mwana wa Ahiludi alikuwa mwandishi wa kumbukumbu; Sadoki mwana wa Ahitubu na Abimeleki mwana wa Abiathari walikuwa makuhani; Shavsha alikuwa katibu; Benaya mwana wa Yehoyada alikuwa mkuu wa Wakerethi na Wapelethi; na wana wa Daudi walikuwa maafisa wakuu karibu na mfalme.

1 Mambo ya Nyakati

Fungua msomaji shirikishi ili kubadilisha tafsiri, kurekebisha herufi, na kutia alama mistari — au vinjari mistari kwa mada.

Manukuu ya Maandiko yametoka katika Open Word Bible, ambayo iko katika uwanja wa umma.