1 Mambo ya Nyakati 14
Open Word Bible
Hiramu mfalme wa Tiro alituma wajumbe kwa Daudi, pamoja na magogo ya mierezi, mafundi wa mawe na mafundi seremala, ili wamjengee jumba la kifalme. Ndipo Daudi akajua kwamba BWANA amemwimarisha kuwa mfalme juu ya Israeli, na ameuinua juu sana ufalme wake kwa ajili ya watu wake Israeli.
Huko Yerusalemu Daudi alioa wake wengine, akawa baba wa wana na binti wengine. Majina ya watoto waliozaliwa kwake huko Yerusalemu ni haya: Shamua, Shobabu, Nathani, Sulemani, Ibhari, Elishua, Elpeleti, Noga, Nefegi, Yafia, Elishama, Beeliada na Elifeleti. Habari zilipowafikia Wafilisti kwamba Daudi amepakwa mafuta kuwa mfalme juu ya Israeli wote, jeshi lote la Wafilisti likapanda kumsaka. Lakini Daudi akasikia habari hiyo, akatoka kwenda kukabiliana nao. Basi Wafilisti walikuwa wamekuja wakavamia Bonde la Refaimu. Basi Daudi akamwuliza Mungu, “Je, nipande kupigana na Wafilisti? Je, wewe utawatia mikononi mwangu?” BWANA akamjibu, “Panda, nami nitawatia mikononi mwako.” Basi walipanda Baal-perasimu, naye Daudi akawashinda huko. Akasema, “Mungu amewavunja adui zangu kwa mkono wangu, kama maji yanavyobomoa kingo.” Ndiyo sababu mahali pale paliitwa Baal-perasimu. Wafilisti waliiacha miungu yao huko, na kwa amri ya Daudi ikachomwa moto.
Kwa mara nyingine Wafilisti walivamia bonde hilo. Daudi alipomwuliza Mungu tena, Mungu alimjibu, “Usipande ukiwafuata. Zunguka mbali nao, uwashambulie ukitokea upande wa miti ya balsamu. Mara utakaposikia sauti ya watu wanaotembea juu ya vilele vya miti ya balsamu, toka uende vitani, kwa maana Mungu ametoka akutangulie kulishinda jeshi la Wafilisti.” Daudi alifanya kama vile Mungu alivyomwamuru, nao wakalishinda jeshi la Wafilisti njia yote kutoka Gibeoni mpaka Gezeri. Basi sifa za Daudi zikaenea katika kila nchi, naye BWANA akayafanya mataifa yote yamwogope.
1 Mambo ya Nyakati
Fungua msomaji shirikishi ili kubadilisha tafsiri, kurekebisha herufi, na kutia alama mistari — au vinjari mistari kwa mada.
Manukuu ya Maandiko yametoka katika Open Word Bible, ambayo iko katika uwanja wa umma.