Yoshua 20
Open Word Bible
Kisha BWANA akamwambia Yoshua, “Waambie Waisraeli: ‘Tengeni miji ya makimbilio niliyowaambia habari zake kupitia Musa, ili mtu yeyote amwuaye mtu kwa makosa, bila kukusudia, aweze kukimbilia huko. Miji hiyo itakuwa mahali pa makimbilio kwenu kutokana na mlipiza kisasi wa damu. Mtu aliyeua atakimbilia mmojawapo wa miji hiyo, asimame mahali pa kuingilia lango la mji, na kuwaeleza wazee wa mji ule jambo lake. Kisha watamkaribisha ndani ya mji na kumpa mahali pa kuishi kati yao. Ikiwa mlipiza kisasi wa damu atamfuatia, wazee hawapaswi kumtia mwuaji mikononi mwake, kwa sababu alimpiga jirani yake bila kukusudia, wala hakuwa adui yake hapo kabla. Mwuaji atakaa katika mji ule mpaka atakaposimama mbele ya jumuiya kuhukumiwa, na mpaka kifo cha kuhani mkuu atakayekuwa akihudumu wakati huo. Ndipo mwuaji ataweza kurudi nyumbani katika mji wake mwenyewe na nyumba yake mwenyewe, mji ule alioukimbia.’” Basi walitenga miji hii: Kedeshi katika Galilaya, katika nchi ya milima ya Naftali; Shekemu, katika nchi ya milima ya Efraimu; na Kiriath-arba, yaani Hebroni, katika nchi ya milima ya Yuda. Upande wa mashariki wa Yordani, mkabala na Yeriko, waliweka Beseri nyikani katika uwanda wa juu, kutoka kabila la Reubeni; Ramothi katika Gileadi, kutoka kabila la Gadi; na Golani katika Bashani, kutoka kabila la Manase. Hii ndiyo iliyokuwa miji iliyowekwa kwa ajili ya Waisraeli wote na kwa ajili ya wageni wanaoishi kati yao. Yeyote aliyemwua mtu kwa makosa angeweza kukimbilia huko, asife kwa mkono wa mlipiza kisasi wa damu kabla ya kusimama mbele ya jumuiya kuhukumiwa.
Yoshua
Fungua msomaji shirikishi ili kubadilisha tafsiri, kurekebisha herufi, na kutia alama mistari — au vinjari mistari kwa mada.
Manukuu ya Maandiko yametoka katika Open Word Bible, ambayo iko katika uwanja wa umma.