Mistari ya Biblia Kuhusu Roho Mtakatifu
Roho ni Mungu mwenyewe akaaye pamoja na watu wake na ndani yao — Msaidizi wetu, Mfariji wetu, muhuri wa ukombozi wetu. Yeye humimina upendo wa Mungu mioyoni mwetu, hukuza matunda yake katika maisha yetu, na hutoa karama kwa faida ya kanisa. Aya hizi zitakusaidia kumkaribisha Roho na kwenda hatua kwa hatua pamoja naye.
Roho Mtakatifu
Lakini huyo Msaidizi, yaani, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atamtuma kwenu kwa Jina langu, atawafundisha mambo yote na kuwakumbusha yote niliyowaambia.
Pia msilewe kwa mvinyo, ambamo ndani yake mna upotovu, bali mjazwe Roho.
Naye atakapokuja, atauthibitishia ulimwengu kuhusu dhambi, haki na hukumu.
Kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio watoto wa Mungu.
Atakapokuja huyo Roho wa kweli atawaongoza awatie katika kweli yote. Yeye hatanena kwa ajili yake mwenyewe, bali atanena yale yote atakayosikia, naye atawaonyesha mambo yajayo.
Je, hamjui ya kwamba ninyi wenyewe ni hekalu la Mungu na kwamba Roho wa Mungu anakaa ndani yenu?
Vivyo hivyo, Roho hutusaidia katika udhaifu wetu, kwa sababu hatujui kuomba ipasavyo. Lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa uchungu usioweza kutamkwa.
Yeyote aniaminiye mimi, kama Maandiko yasemavyo, vijito vya maji ya uzima vitatiririka ndani mwake.”
Ninyi pia mliingia ndani ya Kristo mliposikia Neno la kweli, Injili ya wokovu wenu. Mkiisha kuamini, ndani yake mlitiwa muhuri, yaani, Roho Mtakatifu mliyeahidiwa,
Lakini mtapokea nguvu akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu, nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, Uyahudi kote na Samaria, hadi miisho ya dunia.”
Tunda na Karama za Roho
Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole na kiasi. Katika mambo kama haya hakuna sheria.
Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali roho ya nguvu, ya upendo na ya moyo wa kiasi.
Kila mmoja na atumie kipawa chochote alichopewa kuwahudumia wengine, kama mawakili waaminifu wa neema mbalimbali za Mungu.
Nanyi, upako mlioupata kutoka kwake unakaa ndani yenu, wala ninyi hamna haja ya mtu yeyote kuwafundisha. Lakini kama vile upako wake unavyowafundisha kuhusu mambo yote nayo ni kweli wala si uongo, basi kama ulivyowafundisha kaeni ndani yake.
Kuna aina mbalimbali za karama, lakini Roho ni yule yule.
Basi sasa, yanadumu mambo haya matatu: Imani, tumaini na upendo. Lakini lililo kuu miongoni mwa haya matatu ni upendo.
Fuateni upendo na kutaka sana karama za roho, hasa karama ya unabii.
Kwa sababu hii nakukumbusha uchochee ile karama ya Mungu, iliyowekwa ndani yako nilipokuwekea mikono yangu.
Kama vile mwili ulivyo mmoja nao una viungo vingi, navyo viungo vyote vya mwili ingawa ni vingi, ni mwili mmoja, vivyo hivyo na Kristo.