Mistari ya Biblia Kuhusu Neno la Mungu
Neno la Mungu li hai, tena lina nguvu, ni taa ya miguu yetu na chakula ambacho roho zetu ziliumbwa kwa ajili yake. Ladumu milele, latufanya kuwa na hekima, na latukamilisha kwa kila kazi njema. Aya hizi zinawasha upendo kwa ajili ya Maandiko na Mungu anyenenaye.
Kila Andiko limevuviwa na Mungu na lafaa kwa mafundisho, kwa kuwaonya watu makosa yao, kwa kuwaongoza na kwa kuwafundisha katika haki,
Kwa maana Neno la Mungu li hai tena lina nguvu. Lina makali kuliko upanga wowote wenye makali kuwili, hivyo linachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, viungo na mafuta yaliyo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo.
Usiache Kitabu hiki cha Sheria kiondoke kinywani mwako; yatafakari maneno yake usiku na mchana, ili upate kuwa mwangalifu kufanya kila kitu sawasawa na yote yaliyoandikwa ndani yake. Ndipo utakapofanikiwa na kisha utastawi.
Majani hunyauka na maua huanguka, lakini neno la Mungu wetu ladumu milele.”
Tazama jinsi maneno yako yalivyo matamu kwangu, matamu kuliko asali katika kinywa changu!
Lakini Yesu akajibu, “Imeandikwa: ‘Mtu haishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu.’ ”
Kama watoto wachanga, waliozaliwa sasa, yatamanini maziwa ya kiroho yasiyochanganywa na kitu kingine chochote, ili kwa hayo mpate kukua katika wokovu,
Kisha Yesu akawaambia wale Wayahudi waliomwamini, “Kama mkidumu katika maneno yangu, mtakuwa wanafunzi wangu kweli kweli.