Mistari ya Biblia Kuhusu Haki, Rehema na Maskini
Mungu wa Biblia hupenda haki na huwatetea maskini, yatima, na mjane. Anawaita watu wake kutenda haki, na kupenda rehema, na kwenda kwa unyenyekevu pamoja naye. Aya hizi zinachochea huruma na tendo kuelekea walio dhaifu.
BWANA hupenda zaidi kuona watu wakitenda yaliyo sawa na ya haki kuliko kutoa dhabihu.
Anayemhurumia maskini anamkopesha BWANA, naye atamlipa kwa yale aliyoyatenda.
Mbele ya Mungu Baba, dini iliyo safi na isiyochafuliwa ni hii: kuwasaidia yatima na wajane katika shida zao, na kujiweka mwenyewe bila doa la ulimwengu.
Usimwonee mgeni anayeishi kwako. Ninyi mnajua kwa uzoefu wenu maisha ya mgeni yalivyo, kwa kuwa ninyi wenyewe mlikuwa wageni katika nchi ya Misri.
BWANA ni ngome iliyo juu milimani kwa wale wanaopondwa, mahali salama pa juu nyakati za taabu.
Wahukumuni kwa haki wanyonge na yatima; watangazeni wanaoteseka na fukara kuwa hawana hatia.
Anayemwonea maskini humtukana yule aliyemuumba, bali kumhurumia mhitaji ni kumheshimu yeye.
Watu wakarimu watabarikiwa, kwa sababu huwagawia maskini chakula chao.
“Roho wa Bwana anakaa juu yangu, kwa kuwa amenipaka mafuta ili niwapelekee maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kwamba wako huru, na vipofu kwamba wataona tena, kuwaweka huru wanaokandamizwa,
Fungua kinywa chako kwa ajili ya wale wasio na sauti, kwa ajili ya shauri la wote walioachwa waangamie. Sema waziwazi na uhukumu kwa haki; chukua shauri la maskini na la mhitaji.”
Mfalme atawajibu, ‘Kweli nawaambia, kila mara mlipomfanyia jambo hilo mmoja wa hawa ndugu zangu, hata yule mdogo kuliko wote, mlinifanyia mimi.’