Isaya 65
Neno: Kiswahili Contemporary Version
1“Nilijifunua kwa watu wale ambao hawakuniulizia. Nimeonekana na watu wale ambao hawakunitafuta. Kwa taifa lile ambalo halikuliita Jina langu, nilisema, ‘Niko hapa, niko hapa.’
2Mchana kutwa nimeinyoosha mikono yangu kwa watu wakaidi, wanaokwenda katika njia ambazo si nzuri, wafuatao mawazo yao wenyewe:
3taifa ambalo daima hunikasirisha machoni pangu, wakitoa dhabihu katika bustani na kufukiza uvumba juu ya madhabahu za matofali;
4watu waketio katikati ya makaburi na kukesha mahali pa siri, walao nyama za nguruwe, nazo sufuria zao zina mchuzi wa nyama zilizo najisi,
5wasemao, ‘Kaa mbali; usinikaribie, kwa maana mimi ni mtakatifu mno kwako!’ Watu wa aina hiyo ni moshi katika pua zangu, ni moto uwakao mchana kutwa.
6“Tazama, jambo hili hubakia limeandikwa mbele zangu: sitanyamaza, bali nitalipiza kwa ukamilifu; nitalipiza mapajani mwao:
7dhambi zenu na dhambi za baba zenu,” asema Bwana. “Kwa sababu walitoa dhabihu za kuteketezwa juu ya milima na kunichokoza mimi juu ya vilima, nitawapimia mapajani mwao malipo makamilifu kwa matendo yao ya zamani.”
8Hili ndilo asemalo Bwana: “Kama vile divai mpya ingali bado inapatikana katika kishada cha zabibu, nao watu husema, ‘Usikiharibu, kwa kuwa bado kuna kitu kizuri ndani yake,’ hivyo ndivyo nitakavyofanya kwa ajili ya watumishi wangu; sitawaangamiza wote.
9Nitawaleta wazao kutoka kwa Yakobo, na kutoka kwa Yuda wale watakaomiliki milima yangu, nao watu wangu wateule watairithi, nako huko wataishi watumishi wangu.
10Sharoni itakuwa malisho kwa ajili ya makundi ya kondoo, na Bonde la Akori mahali pa kupumzikia kwa makundi ya ngʼombe, kwa ajili ya watu wangu wanaonitafuta.
11“Bali kwenu ninyi mnaomwacha Bwana na kuusahau mlima wangu mtakatifu, ninyi mnaoandaa meza kwa ajili ya Bahati, na kujaza mabakuli ya mvinyo uliochanganywa kwa ajili ya Ajali,
12nitawaagiza mfe kwa upanga, nanyi nyote mtainama chini ili kuchinjwa; kwa kuwa niliwaita lakini hamkuitika, nilisema lakini hamkusikiliza. Mlitenda maovu machoni pangu, nanyi mkachagua mambo yale yanayonichukiza.”
13Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana Mwenyezi: “Watumishi wangu watakula, lakini ninyi mtaona njaa; watumishi wangu watakunywa lakini ninyi mtaona kiu; watumishi wangu watafurahi, lakini ninyi mtaona haya.
14Watumishi wangu wataimba kwa furaha ya mioyo yao, lakini ninyi mtalia kutokana na uchungu wa moyoni, na kupiga yowe kwa sababu ya uchungu wa roho zenu.
15Mtaliacha jina lenu kuwa laana kwa watu wangu waliochaguliwa; Bwana Mwenyezi atawaua ninyi, lakini watumishi wake atawapa jina jingine.
16Yeye aombaye baraka katika nchi atafanya hivyo kwa Mungu wa kweli; yeye aapaye katika nchi ataapa kwa Mungu wa kweli. Kwa kuwa taabu za zamani zitasahaulika na kufichwa kutoka machoni pangu.
17“Tazama, nitaumba mbingu mpya na dunia mpya. Mambo ya zamani hayatakumbukwa, wala hayatakuja akilini.
18Lakini furahini na kushangilia daima katika hivi nitakavyoumba, kwa kuwa nitaumba Yerusalemu uwe wa kupendeza, nao watu wake wawe furaha.
19Nami nitaifurahia Yerusalemu na kuwafurahia watu wangu; sauti ya maombolezo na ya kilio haitasikika humo tena.
20“Kamwe hatakuwepo tena ndani yake mtoto mchanga atakayeishi siku chache tu, au mzee ambaye hataishi akatimiza miaka yake. Yeye atakayekufa akiwa na umri wa miaka mia moja atahesabiwa kwamba ni kijana tu, yeye ambaye hatafika miaka mia moja, atahesabiwa kuwa amelaaniwa.
21Watajenga nyumba na kuishi ndani yake; watapanda mashamba ya mizabibu na kula matunda yake.
22Hawatajenga nyumba, nao watu wengine waishi ndani yake, au kupanda mazao na wengine wale. Kwa kuwa kama zilivyo siku za mti, ndivyo zitakavyokuwa siku za watu wangu, wateule wangu watafurahia kwa siku nyingi kazi za mikono yao.
23Hawatajitaabisha kwa kazi bure, wala hawatazaa watoto ili wapatwe na majanga, kwa kuwa watakuwa taifa lililobarikiwa na Bwana, wao na wazao wao pamoja nao.
24Kabla hawajaita, nitajibu, nao wakiwa katika kunena, nitasikia.
25Mbwa mwitu na mwana-kondoo watalisha pamoja, naye simba atakula nyasi kama maksai, lakini mavumbi yatakuwa chakula cha nyoka. Hawatadhuru wala kuharibu katika mlima wangu mtakatifu wote,” asema Bwana.
Isaya
Open the interactive reader to switch translations, adjust type, and mark verses — or browse verses by topic.
Neno: Bibilia Takatifu — Kiswahili Contemporary Version. Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. Used under the Biblica Open (Toleo Wazi) License. · Biblica Open License