Isaya 15
Neno: Kiswahili Contemporary Version
1Neno kuhusu Moabu: Ari iliyo Moabu imeangamizwa: imeharibiwa kwa usiku mmoja! Kiri iliyo Moabu imeangamizwa, imeharibiwa kwa usiku mmoja!
2Diboni anakwea hadi kwenye hekalu lake, mpaka mahali pake pa juu ili walie, Moabu anaombolezea Nebo na Medeba. Kila kichwa kimenyolewa na kila ndevu limeondolewa.
3Wamevaa nguo za magunia barabarani, juu ya mapaa na kwenye viwanja wote wanaomboleza, wamelala kifudifudi kwa kulia.
4Heshboni na Eleale wanalia, sauti zao zinasikika hadi Yahazi. Kwa hiyo watu wenye silaha wa Moabu wanapiga kelele, nayo mioyo yao imezimia.
5Moyo wangu unamlilia Moabu; wakimbizi wake wanakimbilia Soari, hadi Eglath-Shelishiya. Wanapanda njia ya kwenda Luhithi, wanakwenda huku wanalia; barabarani iendayo Horonaimu wanaombolezea maangamizi yao.
6Maji ya Nimrimu yamekauka na majani yamenyauka; mimea imekauka wala hakuna kitu chochote kibichi kilichobaki.
7Kwa hiyo mali waliyoipata na kujiwekea akiba wamezichukua na kuvuka Bonde la Mierebi.
8Mwangwi wa kilio chao umefika hadi mpakani mwa Moabu, kilio chao cha huzuni kimefika hadi Eglaimu, maombolezo yao hadi Beer-Elimu.
9Maji ya Dimoni yamejaa damu, lakini bado nitaleta pigo jingine juu ya Dimoni: simba juu ya wakimbizi wa Moabu na juu ya wale wanaobaki katika nchi.
Isaya
Open the interactive reader to switch translations, adjust type, and mark verses — or browse verses by topic.
Neno: Bibilia Takatifu — Kiswahili Contemporary Version. Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. Used under the Biblica Open (Toleo Wazi) License. · Biblica Open License