Isaya 13
Neno: Kiswahili Contemporary Version
1Neno kuhusu Babeli ambalo Isaya mwana wa Amozi aliliona:
2Twekeni bendera juu ya mlima usio na kitu, wapazieni sauti, wapungieni mkono waingie katika malango ya wenye heshima.
3Nimewaamuru watakatifu wangu; nimewaita mashujaa wangu waitimize hasira yangu: wale wanaoshangilia ushindi wangu.
4Sikilizeni kelele juu ya milima, kama ile ya umati mkubwa wa watu! Sikilizeni, makelele katikati ya falme, kama mataifa yanayokusanyika pamoja! Bwana Mwenye Nguvu Zote anakusanya jeshi kwa ajili ya vita.
5Wanakuja kutoka nchi za mbali sana, kutoka miisho ya mbingu, Bwana na silaha za ghadhabu yake, kuangamiza nchi yote.
6Ombolezeni, kwa maana siku ya Bwana i karibu, itakuja kama uharibifu kutoka kwa Mwenyezi.
7Kwa sababu ya hili, mikono yote italegea, moyo wa kila mtu utayeyuka.
8Hofu itawakamata, uchungu na maumivu makali yatawashika, watagaagaa kama mwanamke aliye na utungu wa kuzaa. Watatazamana kwa hofu kila mtu na mwenzake, nyuso zao zikiwaka kama moto.
9Tazameni, siku ya Bwana inakuja, siku katili, yenye ghadhabu na hasira kali, kuifanya nchi kuwa ukiwa na kuwaangamiza wenye dhambi waliomo ndani yake.
10Nyota za mbinguni na makundi ya nyota havitatoa mwanga wake. Jua linalochomoza litatiwa giza na mwezi hautatoa nuru yake.
11Nitauadhibu ulimwengu kwa ajili ya uovu wake, waovu kwa ajili ya dhambi zao. Nitakomesha majivuno ya wenye kiburi, na nitakishusha kiburi cha watu wakatili.
12Nitawafanya wanadamu kuwa adimu kuliko dhahabu safi, watakuwa wachache sana kuliko dhahabu ya Ofiri.
13Kwa hiyo nitazifanya mbingu zitetemeke, nayo dunia itatikisika kutoka mahali pake katika ghadhabu ya Bwana Mwenye Nguvu Zote, katika siku ya hasira yake iwakayo.
14Kama swala awindwaye, kama kondoo wasio na mchungaji, kila mmoja atarudi kwa watu wake mwenyewe, kila mmoja atakimbilia nchi yake ya kuzaliwa.
15Yeyote atakayetekwa atapasuliwa tumbo, wote watakaokamatwa watauawa kwa upanga.
16Watoto wao wachanga watavunjwa vipande vipande mbele ya macho yao; nyumba zao zitatekwa na wake zao watatendwa jeuri.
17Tazama, nitawachochea Wamedi dhidi yao, ambao hawajali fedha wala hawafurahii dhahabu.
18Mishale yao itawaangusha vijana, hawatakuwa na huruma kwa watoto wachanga wala hawataangalia watoto kwa huruma.
19Babeli, johari ya falme, utukufu wa kiburi cha Wababeli, itaangushwa na Mungu kama Sodoma na Gomora.
20Hautakaliwa na watu kamwe wala watu hawataishi humo kwa vizazi vyote. Hakuna Mwarabu atakayepiga hema lake huko, hakuna mchungaji atakayepumzisha makundi yake huko.
21Lakini viumbe wa jangwani watalala huko, mbweha watajaza nyumba zake, bundi wataishi humo nao mbuzi-mwitu watarukaruka humo.
22Fisi watalia ndani ya ngome zake, mbweha ndani ya majumba yake ya kifahari. Wakati wake umewadia, na siku zake hazitaongezwa.
Isaya
Open the interactive reader to switch translations, adjust type, and mark verses — or browse verses by topic.
Neno: Bibilia Takatifu — Kiswahili Contemporary Version. Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. Used under the Biblica Open (Toleo Wazi) License. · Biblica Open License