Isaya 52

Neno: Kiswahili Contemporary Version

1Amka, amka, ee Sayuni, jivike nguvu. Vaa mavazi yako ya fahari, ee Yerusalemu, mji mtakatifu. Asiyetahiriwa na aliye najisi hataingia kwako tena.

2Jikungʼute mavumbi yako, inuka, uketi kwenye kiti cha enzi, ee Yerusalemu. Jifungue minyororo iliyo shingoni mwako, ee Binti Sayuni uliye mateka.

3Kwa kuwa hili ndilo asemalo Bwana: “Mliuzwa pasipo malipo, nanyi mtakombolewa bila fedha.”

4Kwa maana hili ndilo asemalo Bwana Mwenyezi: “Hapo kwanza watu wangu walishuka Misri kuishi, hatimaye, Ashuru wakawaonea.

5“Basi sasa nina nini hapa?” asema Bwana. “Kwa kuwa watu wangu wamechukuliwa pasipo malipo, nao wale wanaowatawala wanawadhihaki,” asema Bwana. “Mchana kutwa jina langu limetukanwa bila kikomo.

6Kwa hiyo watu wangu watalijua Jina langu; kwa hiyo katika siku ile watajua kwamba ndimi niliyetangulia kulisema. Naam, ni mimi.”

7Tazama jinsi miguu ya wale waletao habari njema ilivyo mizuri juu ya milima, wale wanaotangaza amani, wanaoleta habari njema, wanaotangaza wokovu, wauambiao Sayuni, “Mungu wako anatawala!”

8Sikiliza! Walinzi wako wanapaza sauti zao, pamoja wanapaza sauti zao kwa furaha. Wakati Bwana atakaporejea Sayuni, wataliona kwa macho yao wenyewe.

9Pazeni sauti ya nyimbo za furaha pamoja, enyi magofu ya Yerusalemu, kwa maana Bwana amewafariji watu wake, ameikomboa Yerusalemu.

10Mkono mtakatifu wa Bwana umefunuliwa machoni pa mataifa yote, nayo miisho yote ya dunia itaona wokovu wa Mungu wetu.

11Ondokeni, ondokeni, tokeni huko! Msiguse kitu chochote kilicho najisi! Tokeni kati yake mwe safi, ninyi mchukuao vyombo vya Bwana.

12Lakini hamtaondoka kwa haraka, wala hamtakwenda kwa kukimbia; kwa maana Bwana atatangulia mbele yenu, Mungu wa Israeli atakuwa mlinzi nyuma yenu.

13Tazama, mtumishi wangu atatenda kwa hekima; atatukuzwa, na kuinuliwa juu, na kukwezwa sana.

14Kama walivyokuwa wengi walioshangazwa naye, kwani uso wake ulikuwa umeharibiwa sana zaidi ya mtu yeyote na umbo lake kuharibiwa zaidi ya mfano wa mwanadamu:

15hivyo atayashangaza mataifa mengi, nao wafalme watafunga vinywa vyao kwa sababu yake. Kwa kuwa yale ambayo hawakuambiwa, watayaona, nayo yale wasiyoyasikia, watayafahamu.

Isaya

Open the interactive reader to switch translations, adjust type, and mark verses — or browse verses by topic.

Neno: Bibilia Takatifu — Kiswahili Contemporary Version. Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. Used under the Biblica Open (Toleo Wazi) License. · Biblica Open License