Isaya 62
Neno: Kiswahili Contemporary Version
1Kwa ajili ya Sayuni sitanyamaza, kwa ajili ya Yerusalemu sitatulia, mpaka haki yake itakapoangaza kama mapambazuko, wokovu wake kama mwanga wa moto.
2Mataifa wataona haki yako, nao wafalme wote wataona utukufu wako; wewe utaitwa kwa jina jipya lile ambalo kinywa cha Bwana kitatamka.
3Utakuwa taji ya fahari mkononi mwa Bwana, taji ya kifalme mkononi mwa Mungu wako.
4Hawatakuita tena Aliyeachwa, wala nchi yako kuiita Ukiwa. Bali utaitwa Hefsiba, nayo nchi yako itaitwa Beula, kwa maana Bwana atakufurahia, nayo nchi yako itaolewa.
5Kama vile kijana aoavyo mwanamwali, ndivyo wanao watakavyokuoa wewe; kama bwana arusi amfurahiavyo bibi arusi wake, ndivyo Mungu wako atakavyokufurahia wewe.
6Nimeweka walinzi juu ya kuta zako, ee Yerusalemu, hawatanyamaza mchana wala usiku. Ninyi wenye kumwita Bwana, msitulie,
7msimwache apumzike hadi atakapoufanya imara Yerusalemu na kuufanya uwe sifa ya dunia.
8Bwana ameapa kwa mkono wake wa kuume na kwa mkono wake wenye nguvu: “Kamwe sitawapa tena adui zenu nafaka zenu kama chakula chao; kamwe wageni hawatakunywa tena divai mpya ambayo mmeitaabikia,
9lakini wale waivunao nafaka wataila na kumsifu Bwana, nao wale wakusanyao zabibu watainywa divai yake katika nyua za patakatifu pangu.”
10Piteni, piteni katika malango! Tengenezeni njia kwa ajili ya watu. Jengeni, jengeni njia kuu! Ondoeni mawe. Inueni bendera kwa ajili ya mataifa.
11Bwana ametoa tangazo mpaka miisho ya dunia: “Mwambie Binti Sayuni, ‘Tazama, mwokozi wako anakuja! Tazama ujira wake uko pamoja naye, na malipo yake yanafuatana naye!’ ”
12Wataitwa Watu Watakatifu, Waliokombolewa na Bwana; nawe utaitwa Aliyetafutwa, Mji Usioachwa Tena.
Isaya
Open the interactive reader to switch translations, adjust type, and mark verses — or browse verses by topic.
Neno: Bibilia Takatifu — Kiswahili Contemporary Version. Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. Used under the Biblica Open (Toleo Wazi) License. · Biblica Open License