Isaya 14

Neno: Kiswahili Contemporary Version

1Bwana atamhurumia Yakobo, atamchagua Israeli tena, na kuwakalisha katika nchi yao wenyewe. Wageni wataungana nao na kujiunga na nyumba ya Yakobo.

2Mataifa watawachukua na kuwaleta mahali pao wenyewe. Nayo nyumba ya Israeli itamiliki mataifa kama watumishi na wajakazi katika nchi ya Bwana. Watawafanya watekaji wao kuwa mateka, na kutawala juu ya wale waliowaonea.

3Katika siku Bwana atakapokuondolea mateso, udhia na utumwa wa kikatili,

4utaichukua dhihaka hii dhidi ya mfalme wa Babeli: Tazama jinsi mtesi alivyofikia mwisho! Tazama jinsi ghadhabu yake kali ilivyokoma!

5Bwana amevunja fimbo ya mwovu, fimbo ya utawala ya watawala,

6ambayo kwa hasira waliyapiga mataifa kwa mapigo yasiyo na kikomo, nao kwa ghadhabu kali waliwatiisha mataifa kwa jeuri pasipo huruma.

7Nchi zote ziko kwenye mapumziko na kwenye amani, wanabubujika kwa kuimba.

8Hata misunobari na mierezi ya Lebanoni inashangilia mbele yako na kusema, “Basi kwa sababu umeangushwa chini, hakuna mkata miti atakayekuja kutukata.”

9Kuzimu kote kumetaharuki kukulaki unapokuja, kunaamsha roho za waliokufa ili kukupokea, wote waliokuwa viongozi katika ulimwengu, kunawafanya wainuke kwenye viti vyao vya kifalme: wale wote waliokuwa wafalme juu ya mataifa.

10Wote wataitikia, watakuambia, “Wewe pia umekuwa dhaifu, kama sisi tulivyo; wewe umekuwa kama sisi.”

11Majivuno yako yote yameshushwa mpaka kuzimu, pamoja na kelele ya vinubi vyako, mafunza yametanda chini yako, na minyoo imekufunika.

12Tazama jinsi ulivyoanguka kutoka mbinguni, ewe nyota ya asubuhi, mwana wa mapambazuko! Umetupwa chini duniani, wewe uliyepata kuangusha mataifa!

13Ulisema moyoni mwako, “Nitapanda juu hadi mbinguni, nitakiinua kiti changu cha enzi juu ya nyota za Mungu, nitaketi nimetawazwa juu ya mlima wa kusanyiko, kwenye vimo vya juu sana vya Mlima Mtakatifu.

14Nitapaa juu kupita mawingu, nitajifanya kama Yeye Aliye Juu Sana.”

15Lakini umeshushwa chini hadi kuzimu, hadi kwenye vina vya shimo.

16Wale wanaokuona wanakukazia macho, wanatafakari hatima yako: “Je, huyu ndiye yule aliyetikisa dunia na kufanya falme zitetemeke,

17yule aliyeifanya dunia kuwa jangwa, aliyeipindua miji yake, na ambaye hakuwaachia mateka wake waende nyumbani?”

18Wafalme wote wa mataifa wamelala kwa heshima kila mmoja katika kaburi lake.

19Lakini wewe umetupwa nje ya kaburi lako kama tawi lililokataliwa, umefunikwa na waliouawa pamoja na wale waliochomwa kwa upanga, wale washukao mpaka kwenye mawe ya shimo. Kama mzoga uliokanyagwa chini ya nyayo,

20Hutajumuika nao kwenye mazishi, kwa kuwa umeharibu nchi yako na kuwaua watu wako. Mzao wa mwovu hatatajwa tena kamwe.

21Andaa mahali pa kuwachinjia wanawe kwa ajili ya dhambi za baba zao, wasije wakainuka ili kuirithi nchi na kuijaza dunia kwa miji yao.

22Bwana Mwenye Nguvu Zote asema, “Nitainuka dhidi yao, nitalikatilia mbali jina lake kutoka Babeli pamoja na watu wake walionusurika, watoto wake na wazao wake,” asema Bwana.

23“Nitaifanya kuwa mahali pa bundi, na kuwa nchi ya matope; nitaifagia kwa ufagio wa maangamizi,” asema Bwana Mwenye Nguvu Zote.

24Bwana Mwenye Nguvu Zote ameapa, “Hakika, kama vile nilivyopanga, ndivyo itakavyokuwa, nami kama nilivyokusudia, ndivyo itakavyosimama.

25Nitamponda Mwashuru katika nchi yangu, juu ya milima yangu nitawakanyagia chini. Nira yake itaondolewa kutoka kwa watu wangu, nao mzigo wake utaondolewa kutoka mabegani mwao.”

26Huu ndio mpango uliokusudiwa kwa ajili ya ulimwengu wote, huu ni mkono ulionyooshwa juu ya mataifa yote.

27Kwa kuwa Bwana Mwenye Nguvu Zote amekusudia, ni nani awezaye kumzuia? Mkono wake umenyooshwa, ni nani awezaye kuurudisha?

28Neno hili lilikuja mwaka ule Mfalme Ahazi alipofariki:

29Msifurahi, enyi Wafilisti wote, kwamba fimbo iliyowapiga imevunjika; kutoka mzizi wa huyo nyoka atachipuka nyoka mwenye sumu kali, uzao wake utakuwa joka lirukalo, lenye sumu kali.

30Maskini kuliko maskini wote watapata malisho, nao wahitaji watalala salama. Lakini mzizi wako nitauangamiza kwa njaa, nayo njaa itawaua walionusurika.

31Piga yowe, ee lango! Bweka, ee mji! Yeyukeni, enyi Wafilisti wote! Wingu la moshi linakuja toka kaskazini, wala hakuna atakayechelewa katika safu zake.

32Ni jibu gani litakalotolewa kwa wajumbe wa taifa hilo? “ Bwana ameifanya imara Sayuni, nako ndani yake watu wake walioonewa watapata kimbilio.”

Isaya

Open the interactive reader to switch translations, adjust type, and mark verses — or browse verses by topic.

Neno: Bibilia Takatifu — Kiswahili Contemporary Version. Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. Used under the Biblica Open (Toleo Wazi) License. · Biblica Open License