Isaya 27
Neno: Kiswahili Contemporary Version
1Katika siku ile, Bwana ataadhibu kwa upanga wake, upanga wake mkali, mkubwa na wenye nguvu, ataadhibu Lewiathani yule nyoka apitaye kwa mwendo laini, Lewiathani yule nyoka mwenye kujipinda; atamuua joka huyo mkubwa sana wa baharini.
2Katika siku ile: “Imbeni kuhusu shamba la mizabibu lililozaa:
3Mimi, Bwana, ninalitunza, nalinyweshea maji mfululizo. Ninalichunga usiku na mchana ili mtu yeyote asije akalidhuru.
4Mimi sijakasirika. Licha pangekuwepo michongoma na miiba kunikabili! Ningepambana dhidi yake katika vita, ningeliichoma moto yote.
5Au niwaache waje kwangu kwa ajili ya kupata kimbilio, wao na wafanye amani nami, naam, wafanye amani nami.”
6Katika siku zijazo, Yakobo atatia mizizi, Israeli atatoa chipukizi na kuchanua maua, naye atajaza ulimwengu wote kwa matunda.
7Je, Bwana amempiga vile alivyowapiga wale waliompiga? Je, yeye ameuawa vile walivyouawa wale waliomuua yeye?
8Kwa vita na kwa kumfukuza unapingana naye: kwa mshindo wake mkali anamfukuza, kama siku ile uvumapo upepo wa mashariki.
9Kwa hili, basi, hatia ya Yakobo itafanyiwa upatanisho, nalo hili litakuwa matunda ya utimilizo wa kuondolewa kwa dhambi yake: Wakati atakapoyafanya mawe yote ya madhabahu kuwa kama mawe ya chokaa yaliyopondwa vipande vipande, hakuna nguzo za Ashera au madhabahu za kufukizia uvumba zitakazobaki zimesimama.
10Mji ulio na boma umebaki ukiwa, makao yaliyotelekezwa, yaliyoachwa kama jangwa. Huko ndama hulisha, huko hujilaza, wanakwanyua matawi yake.
11Wakati vijiti vyake vimekauka, huvunjwa nao wanawake huja na kuwasha navyo moto. Kwa kuwa hili ni taifa lisilo na ufahamu, kwa hiyo yeye aliyewafanya hana huruma juu yao, Muumba wao hawaonyeshi fadhili.
12Katika siku ile Bwana atapura kutoka matiririko ya Mto Frati hadi Kijito cha Misri, nanyi ee Waisraeli, mtakusanywa mmoja mmoja.
13Katika siku ile tarumbeta kubwa italia. Wale waliokuwa wakiangamia katika nchi ya Ashuru, nao wale waliokuwa uhamishoni katika nchi ya Misri watakuja na kumwabudu Bwana katika mlima mtakatifu huko Yerusalemu.
Isaya
Open the interactive reader to switch translations, adjust type, and mark verses — or browse verses by topic.
Neno: Bibilia Takatifu — Kiswahili Contemporary Version. Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. Used under the Biblica Open (Toleo Wazi) License. · Biblica Open License