Isaya 24
Neno: Kiswahili Contemporary Version
1Tazama, Bwana ataifanya dunia kuwa ukiwa na kuiharibu, naye atauharibu uso wake na kutawanya wakaao ndani yake:
2ndivyo itakavyokuwa kwa makuhani na kwa watu, kwa bwana na kwa mtumishi, kwa bibi na kwa mtumishi wake wa kike, kwa muuzaji na kwa mnunuzi, kwa mkopaji na kwa mkopeshaji, kwa mdaiwa na kwa mdai.
3Dunia itaharibiwa kabisa na kutekwa nyara kabisa. Bwana amesema neno hili.
4Dunia inakauka na kunyauka, dunia inanyongʼonyea na kunyauka, waliotukuzwa wa dunia wananyongʼonyea.
5Dunia imetiwa unajisi na watu wake; wameacha kutii sheria, wamevunja amri na kuvunja agano la milele.
6Kwa hiyo laana inaiteketeza dunia, watu wake lazima waichukue hatia yao. Kwa hiyo wakazi wa dunia wameteketezwa, nao waliosalia ni wachache sana.
7Divai mpya inakauka na mzabibu unanyauka, watu wote wafurahishao wanalia kwa huzuni.
8Furaha ya matoazi imekoma, kelele za wenye furaha zimekoma, shangwe za kinubi zimenyamaza.
9Hawanywi tena mvinyo pamoja na wimbo, kileo ni kichungu kwa wanywaji wake.
10Mji ulioharibiwa umekuwa ukiwa, mlango wa kila nyumba umefungwa.
11Barabarani wanalilia kupata mvinyo, furaha yote imegeuka kuwa majonzi, furaha yote imefukuziwa mbali na dunia.
12Mji umeachwa katika uharibifu, lango lake limevunjwa vipande.
13Ndivyo itakavyokuwa duniani na miongoni mwa mataifa, kama vile wakati mzeituni upigwavyo, au kama vile wakati masazo yabakiavyo baada ya zabibu kuvunwa.
14Wanainua sauti zao, wanapiga kelele kwa furaha, kutoka magharibi wanasifu kwa ukelele utukufu wa Bwana.
15Kwa hiyo upande wa mashariki mpeni Bwana utukufu, liadhimisheni jina la Bwana, Mungu wa Israeli, katika visiwa vya bahari.
16Kutoka miisho ya dunia tunasikia uimbaji: “Utukufu kwa Yule Mwenye Haki.” Lakini nilisema, “Ninadhoofika, ninadhoofika! Ole wangu! Watenda hila wanasaliti! Kwa hila watenda hila wanasaliti!”
17Hofu, shimo na mtego vinakungojea, ewe mtu ukaaye duniani.
18Kila akimbiaye asikiapo sauti ya hofu atatumbukia shimoni, naye yeyote apandaye kutoka shimoni, atanaswa kwenye mtego. Malango ya gharika ya mbinguni yamefunguliwa, misingi ya dunia inatikisika.
19Dunia imepasuka, dunia imechanika, dunia imetikiswa kabisa.
20Dunia inapepesuka kama mlevi, inayumbayumba kama kibanda kwenye upepo; imelemewa sana na mzigo wa hatia ya uasi wake na ikianguka kamwe haitainuka tena.
21Katika siku ile Bwana ataadhibu nguvu zilizoko mbinguni juu, na wafalme walioko duniani chini.
22Watakusanywa pamoja kama wafungwa waliofungwa gerezani, watafungiwa gerezani na kuadhibiwa baada ya siku nyingi.
23Mwezi utatiwa haya, nalo jua litaaibishwa; kwa maana Bwana Mwenye Nguvu Zote atawala juu ya Mlima Sayuni na katika Yerusalemu, tena mbele ya wazee wake kwa utukufu.
Isaya
Open the interactive reader to switch translations, adjust type, and mark verses — or browse verses by topic.
Neno: Bibilia Takatifu — Kiswahili Contemporary Version. Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. Used under the Biblica Open (Toleo Wazi) License. · Biblica Open License