Isaya 55
Neno: Kiswahili Contemporary Version
1“Njooni, ninyi nyote wenye kiu, njooni kwenye maji; nanyi ambao hamna fedha, njooni, nunueni na mle! Njooni, nunueni divai na maziwa bila fedha na bila gharama.
2Kwa nini kutumia fedha kwa kitu ambacho si chakula, na kutaabikia kitu kisichoshibisha? Sikilizeni, nisikilizeni mimi na mle kilicho kizuri, nazo nafsi zenu zitafurahia utajiri wa unono.
3Tegeni sikio mje kwangu, nisikieni mimi, ili nafsi zenu zipate kuishi. Nitafanya agano la milele nanyi, pendo la uaminifu nililomwahidi Daudi.
4Tazama, nimemfanya kuwa shahidi wa mataifa, kiongozi na jemadari wa mataifa.
5Hakika utaita mataifa usiyoyajua, nayo mataifa yale yasiyokujua yataharakisha kukujia, kwa sababu ya Bwana Mungu wako, yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli, kwa maana amekutukuza.”
6Mtafuteni Bwana maadamu anapatikana; mwiteni maadamu yu karibu.
7Mtu mwovu na aiache njia yake, na mtu mbaya na ayaache mawazo yake. Yeye na amrudie Bwana, naye atamrehemu, arudi kwa Mungu wetu, kwa kuwa atamsamehe bure kabisa.
8“Kwa kuwa mawazo yangu si mawazo yenu, wala njia zenu si njia zangu,” asema Bwana.
9“Kama vile mbingu zilivyo juu kuliko dunia, ndivyo njia zangu zilivyo juu kuliko njia zenu na mawazo yangu kuliko mawazo yenu.
10Kama vile mvua na theluji ishukavyo kutoka mbinguni, nayo hairudi tena huko bila kunywesha dunia na kuichipusha na kuistawisha, hivyo hutoa mbegu kwa mpanzi na mkate kwa mlaji,
11ndivyo lilivyo neno langu lile litokalo kinywani mwangu: Halitanirudia tupu, bali litatimiliza lile nililokusudia na litafanikiwa katika kusudi lile nililolituma.
12Mtatoka nje kwa furaha na kuongozwa kwa amani; milima na vilima vitapaza sauti kwa nyimbo mbele yenu, nayo miti yote ya shambani itapiga makofi.
13Badala ya kichaka cha miiba itaota miti ya misunobari, na badala ya michongoma utaota mhadasi. Hili litakuwa jambo la kumpatia Bwana jina, kwa ajili ya ishara ya milele, ambayo haitaharibiwa.”
Isaya
Open the interactive reader to switch translations, adjust type, and mark verses — or browse verses by topic.
Neno: Bibilia Takatifu — Kiswahili Contemporary Version. Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. Used under the Biblica Open (Toleo Wazi) License. · Biblica Open License