Maombolezo 1
Neno: Kiswahili Contemporary Version
1Tazama jinsi mji ulivyoachwa ukiwa, mji ambao zamani ulikuwa umejaa watu! Jinsi ambavyo umekuwa kama mama mjane, ambaye wakati fulani alikuwa maarufu miongoni mwa mataifa! Yule ambaye alikuwa malkia miongoni mwa majimbo sasa amekuwa mtumwa.
2Kwa uchungu, hulia sana usiku, machozi yapo kwenye mashavu yake. Miongoni mwa wapenzi wake wote hakuna yeyote wa kumfariji. Rafiki zake wote wamemsaliti, wamekuwa adui zake.
3Baada ya mateso na kufanyishwa kazi kikatili, Yuda amekwenda uhamishoni. Anakaa miongoni mwa mataifa, hapati mahali pa kupumzika. Wote ambao wanamsaka wamemkamata katikati ya dhiki yake.
4Barabara zielekeazo Sayuni zaomboleza, kwa kuwa hakuna yeyote anayekuja kwenye sikukuu zake zilizoamriwa. Malango yake yote yamekuwa ukiwa, makuhani wake wanalia kwa uchungu, wanawali wake wanahuzunika, naye yuko katika uchungu wa maumivu makuu.
5Adui zake wamekuwa mabwana zake, watesi wake wana raha. Bwana amemletea huzuni kwa sababu ya dhambi zake nyingi. Watoto wake wamekwenda uhamishoni, mateka mbele ya adui.
6Fahari yote imeondoka kutoka kwa Binti Sayuni. Wakuu wake wako kama ayala ambaye hapati malisho, katika udhaifu wamekimbia mbele ya anayewasaka.
7Katika siku za mateso yake na kutangatanga, Yerusalemu hukumbuka hazina zote ambazo zilikuwa zake siku za kale. Wakati watu wake walipoanguka katika mikono ya adui, hapakuwepo na yeyote wa kumsaidia. Watesi wake walimtazama na kumcheka katika maangamizi yake.
8Yerusalemu ametenda dhambi sana kwa hiyo amekuwa najisi. Wote waliomheshimu wanamdharau, kwa maana wameuona uchi wake. Yeye mwenyewe anapiga kite na kugeukia mbali.
9Uchafu wake umegandamana na nguo zake; hakuwaza juu ya maisha yake ya baadaye. Anguko lake lilikuwa la kushangaza, hapakuwepo na yeyote wa kumfariji. “Tazama, Ee Bwana, teso langu, kwa maana adui ameshinda.”
10Adui ametia mikono juu ya hazina zake zote, aliona mataifa ya kipagani wakiingia mahali patakatifu pake, wale uliowakataza kuingia kwenye kusanyiko lako.
11Watu wake wote wanalia kwa uchungu watafutapo chakula; wanabadilisha hazina zao kwa chakula ili waweze kuendelea kuishi. “Tazama, Ee Bwana, ufikiri, kwa maana nimedharauliwa.”
12“Je, si kitu kwenu, ninyi nyote mpitao kando? Angalieni kote mwone. Je, kuna maumivu kama maumivu yangu yale yaliyotiwa juu yangu, yale Bwana aliyoyaleta juu yangu katika siku ya hasira yake kali?
13“Kutoka juu alipeleka moto, akaushusha katika mifupa yangu. Aliitandia wavu miguu yangu na akanirudisha nyuma. Akanifanya mkiwa, na mdhaifu mchana kutwa.
14“Dhambi zangu zimefungwa kwenye nira, kwa mikono yake zilifumwa pamoja. Zimefika shingoni mwangu na Bwana ameziondoa nguvu zangu. Amenitia mikononi mwa wale ambao siwezi kushindana nao.
15“Bwana amewakataa wapiganaji wa vita wote walio kati yangu, ameagiza jeshi dhidi yangu kuwaponda vijana wangu wa kiume. Katika shinikizo lake la divai Bwana amemkanyaga Bikira Binti Yuda.
16“Hii ndiyo sababu ninalia na macho yangu yanafurika machozi. Hakuna yeyote aliye karibu kunifariji, hakuna yeyote wa kuhuisha roho yangu. Watoto wangu ni wakiwa kwa sababu adui ameshinda.”
17Sayuni ananyoosha mikono yake, lakini hakuna yeyote wa kumfariji. Bwana ametoa amri kwa ajili ya Yakobo kwamba majirani zake wawe adui zake; Yerusalemu umekuwa kitu najisi miongoni mwao.
18“ Bwana ni mwenye haki, hata hivyo niliasi dhidi ya amri yake. Sikilizeni, enyi mataifa yote, tazameni maumivu yangu. Wavulana wangu na wasichana wangu wamekwenda uhamishoni.
19“Niliita washirika wangu lakini walinisaliti. Makuhani wangu na wazee wangu waliangamia mjini walipokuwa wakitafuta chakula ili waweze kuishi.
20“Angalia, Ee Bwana, jinsi nilivyo katika dhiki! Nina maumivu makali ndani yangu, nami ninahangaika moyoni mwangu, kwa kuwa nimekuwa mwasi sana. Huko nje, upanga unaua watu, ndani, kipo kifo tu.
21“Watu wamesikia ninavyolia kwa uchungu, lakini hakuna yeyote wa kunifariji. Adui zangu wote wamesikia juu ya dhiki yangu, wanafurahia lile ulilolitenda. Naomba uilete siku uliyoitangaza ili wawe kama mimi.
22“Uovu wao wote na uje mbele zako; uwashughulikie wao kama vile ulivyonishughulikia mimi kwa sababu ya dhambi zangu zote. Kulia kwangu kwa uchungu ni kwingi na moyo wangu umedhoofika.”
Maombolezo
Open the interactive reader to switch translations, adjust type, and mark verses — or browse verses by topic.
Neno: Bibilia Takatifu — Kiswahili Contemporary Version. Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. Used under the Biblica Open (Toleo Wazi) License. · Biblica Open License