Maombolezo 3

Neno: Kiswahili Contemporary Version

1Mimi ndiye mtu aliyeona mateso kwa fimbo ya ghadhabu yake.

2Amenifukuzia mbali na kunifanya nitembee gizani wala si katika nuru;

3hakika, amegeuza mkono wake dhidi yangu tena na tena, mchana kutwa.

4Amefanya ngozi yangu na nyama yangu kuchakaa na ameivunja mifupa yangu.

5Amenizingira na kunizunguka kwa uchungu na taabu.

6Amenifanya niishi gizani kama wale waliokufa.

7Amenizungushia ukuta ili nisiweze kutoroka, amenifunga kwa minyororo mizito.

8Hata ninapoita au kulia ili kuomba msaada, anakataa kupokea maombi yangu.

9Ameizuia njia yangu kwa mapande ya mawe, amepotosha njia zangu.

10Kama dubu aviziaye, kama simba mafichoni,

11ameniburuta kutoka njia, akanirarua na kuniacha bila msaada.

12Amevuta upinde wake na kunifanya mimi niwe lengo kwa ajili ya mishale yake.

13Alinichoma moyo wangu kwa mishale iliyotoka kwenye podo lake.

14Nimekuwa kichekesho kwa watu wangu wote, wananidhihaki kwa wimbo mchana kutwa.

15Amenijaza kwa majani machungu na kunishibisha kwa nyongo.

16Amevunja meno yangu kwa changarawe, amenikanyagia mavumbini.

17Amani yangu imeondolewa, nimesahau kufanikiwa ni nini.

18Kwa hiyo nasema, “Fahari yangu imeondoka na yale yote niliyokuwa nimetarajia kutoka kwa Bwana.”

19Nayakumbuka mateso yangu na kutangatanga kwangu, uchungu na nyongo.

20Ninayakumbuka vyema, nayo nafsi yangu imezimia ndani yangu.

21Hata hivyo najikumbusha neno hili na kwa hiyo ninalo tumaini.

22Kwa sababu ya upendo mkuu wa Bwana, hatuangamii, kwa kuwa huruma zake hazikomi kamwe.

23Ni mpya kila asubuhi, uaminifu wako ni mkuu.

24Nimeiambia nafsi yangu, “ Bwana ni fungu langu, kwa hiyo nitamngojea.”

25Bwana ni mwema kwa wale ambao tumaini lao ni kwake, kwa yule ambaye humtafuta;

26ni vyema kungojea kwa utulivu kwa ajili ya wokovu wa Bwana.

27Ni vyema mtu kuchukua nira bado angali kijana.

28Na akae peke yake awe kimya, kwa maana Bwana ameiweka juu yake.

29Na azike uso wake mavumbini bado panawezekana kuwa na matumaini.

30Na atoe shavu lake kwa yule ampigaye, na ajazwe na aibu.

31Kwa kuwa watu hawakatiliwi mbali na Bwana milele.

32Ingawa huleta huzuni, ataonyesha huruma, kwa kuwa upendo wake usiokoma ni mkuu.

33Kwa maana hapendi kuwaletea mateso au huzuni watoto wa wanadamu.

34Kuwaponda chini ya nyayo wafungwa wote katika nchi,

35Kumnyima mtu haki zake mbele za Aliye Juu Sana,

36kumnyima mtu haki: Je, Bwana asione mambo kama haya?

37Nani awezaye kusema nalo likatendeka kama Bwana hajaamuru?

38Je, si ni kwenye kinywa cha Aliye Juu Sana ndiko yatokako maafa na mambo mema?

39Mwanadamu yeyote aliye hai aweza kulalamika wakati anapoadhibiwa kwa ajili ya dhambi zake?

40Tuzichunguze njia zetu na kuzijaribu, na tumrudie Bwana Mungu.

41Tuinue mioyo yetu pamoja na mikono yetu kwa Mungu mbinguni, na tuseme:

42“Tumetenda dhambi na kuasi nawe hujasamehe.

43“Umejifunika mwenyewe kwa hasira na kutufuatilia; umetuchinja bila huruma.

44Unajifunika mwenyewe kwa wingu, ili pasiwe na ombi litakaloweza kupenya.

45Umetufanya takataka na uchafu miongoni mwa mataifa.

46“Adui zetu wote wamefumbua vinywa vyao wazi dhidi yetu.

47Tumeteseka kwa hofu kuu na shida ya ghafula, uharibifu na maangamizi.”

48Vijito vya machozi vinatiririka kutoka machoni mwangu, kwa sababu watu wangu wameangamizwa.

49Macho yangu yatatiririka machozi bila kukoma, bila kupata nafuu,

50hadi Bwana atazame chini kutoka mbinguni na kuona.

51Lile ninaloliona huniletea huzuni nafsini kwa sababu ya wanawake wote wa mji wangu.

52Wale waliokuwa adui zangu bila sababu wameniwinda kama ndege.

53Walijaribu kukomesha maisha yangu ndani ya shimo na kunitupia mawe;

54maji yalifunika juu ya kichwa changu, nami nikafikiri nilikuwa karibu kukatiliwa mbali.

55Nililiitia jina lako, Ee Bwana, kutoka vina vya shimo.

56Ulisikia ombi langu: “Usikizibie masikio yako kilio changu nikuombapo msaada.”

57Ulikuja karibu nilipokuita, nawe ukasema, “Usiogope.”

58Ee Bwana, ulichukua shauri langu, ukaukomboa uhai wangu.

59Umeona, Ee Bwana, ubaya niliotendewa. Tetea shauri langu!

60Umeona kina cha kisasi chao, mashauri yao yote mabaya dhidi yangu.

61Ee Bwana, umesikia matukano yao, mashauri yao yote mabaya dhidi yangu:

62kile adui zangu wanachonongʼona na kunungʼunikia dhidi yangu mchana kutwa.

63Watazame! Wakiwa wameketi au wamesimama, wananidhihaki katika nyimbo zao.

64Uwalipe kile wanachostahili, Ee Bwana, kwa yale ambayo mikono yao imetenda.

65Weka pazia juu ya mioyo yao, laana yako na iwe juu yao!

66Wafuatilie katika hasira na uwaangamize kutoka chini ya mbingu za Bwana.

Maombolezo

Open the interactive reader to switch translations, adjust type, and mark verses — or browse verses by topic.

Neno: Bibilia Takatifu — Kiswahili Contemporary Version. Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. Used under the Biblica Open (Toleo Wazi) License. · Biblica Open License