Maombolezo 4

Neno: Kiswahili Contemporary Version

1Jinsi dhahabu ilivyopoteza mngʼao wake, dhahabu iliyo safi haingʼai! Vito vya thamani vimetawanywa kwenye mwanzo wa kila barabara.

2Wana wa Sayuni wenye thamani, ambao mwanzo uzito wa thamani yao ulikuwa wa dhahabu, sasa wanaangaliwa kama vyungu vya udongo, kazi ya mikono ya mfinyanzi!

3Hata mbweha hutoa matiti yao kunyonyesha watoto wao, lakini watu wangu wamekuwa wasio na huruma kama mbuni jangwani.

4Kwa sababu ya kiu ulimi wa mtoto mchanga umegandamana na kaakaa la kinywa chake, watoto huomba mkate, lakini hakuna yeyote awapaye.

5Wale waliokula vyakula vya kifahari ni maskini barabarani. Wale waliokuzwa wakivaa nguo za zambarau sasa wanalalia majivu.

6Adhabu ya watu wangu ni kubwa kuliko ile ya Sodoma, ambayo ilipinduliwa ghafula bila kuwepo mkono wa msaada.

7Wakuu wao walikuwa wamengʼaa kuliko theluji na weupe kuliko maziwa, miili yao ilikuwa myekundu kuliko marijani, kuonekana kwao kama yakuti samawi.

8Lakini sasa ni weusi kuliko masizi; hawatambulikani barabarani. Ngozi yao imeshikamana juu ya mifupa yao, imekuwa mikavu kama fimbo.

9Wale waliouawa kwa upanga ni bora kuliko wale wanaokufa njaa; wanateseka kwa njaa, wanatokomea kwa kukosa chakula kutoka shambani.

10Kwa mikono yao wenyewe wanawake wenye huruma wanapika watoto wao wenyewe, waliokuwa chakula chao watu wangu walipoangamizwa.

11Bwana ametoa nafasi kamilifu ya ghadhabu yake; ameimwaga hasira yake kali. Amewasha moto katika Sayuni ambao umeteketeza misingi yake.

12Wafalme wa dunia hawakuamini, wala mtu yeyote wa duniani, kwamba adui na watesi wangeweza kuingia kwenye malango ya Yerusalemu.

13Lakini hili lilitokea kwa sababu ya dhambi za manabii wake, na maovu ya makuhani wake, waliomwaga ndani yake damu ya wenye haki.

14Sasa wanapapasa papasa barabarani kama watu ambao ni vipofu. Wamenajisiwa kabisa kwa damu, hata hakuna anayethubutu kugusa mavazi yao.

15Watu wanawapigia kelele, “Ondokeni! Ninyi ni najisi! Ondokeni! Ondokeni! Msituguse!” Wanapokimbia na kutangatanga huku na huko, watu miongoni mwa mataifa wanasema, “Hawawezi kukaa hapa zaidi.”

16Bwana mwenyewe amewatawanya; hawaangalii tena. Makuhani hawaonyeshwi heshima, wazee hawakubaliki.

17Zaidi ya hayo, macho yetu yalichoka, kwa kutazamia bure msaada; tuliangalia kutoka minara yetu kwa taifa lisiloweza kutuokoa.

18Watu walituvizia katika kila hatua hata hatukuweza kutembea katika barabara zetu. Mwisho wetu ulikuwa karibu, siku zetu zilikuwa zimetimia, kwa maana mwisho wetu ulikuwa umefika.

19Waliotufuatia walikuwa wepesi kuliko tai angani; walitusaka juu milimani na kutuvizia jangwani.

20Mpakwa mafuta wa Bwana, pumzi ya uhai wetu hasa, alinaswa katika mitego yao. Tulifikiri kwamba chini ya kivuli chake tungeliweza kuishi miongoni mwa mataifa.

21Shangilia na ufurahi, ee Binti Edomu, wewe unayeishi nchi ya Usi. Lakini kwako pia kikombe kitapitishwa, Utalewa na kuvuliwa nguo ubaki uchi.

22Ee Binti Sayuni, adhabu yako itaisha, hatarefusha muda wako wa kukaa uhamishoni. Lakini, ee Binti Edomu, ataadhibu dhambi yako, na atafunua uovu wako.

Maombolezo

Open the interactive reader to switch translations, adjust type, and mark verses — or browse verses by topic.

Neno: Bibilia Takatifu — Kiswahili Contemporary Version. Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. Used under the Biblica Open (Toleo Wazi) License. · Biblica Open License