Wimbo 8

Neno: Kiswahili Contemporary Version

1Laiti ungelikuwa kwangu kama ndugu wa kiume, ambaye aliyanyonya matiti ya mama yangu! Kisha, kama ningekukuta huko nje, ningelikubusu, wala hakuna mtu yeyote angelinidharau.

2Ningelikuongoza na kukuleta katika nyumba ya mama yangu, yeye ambaye amenifundisha. Ningelikupa divai iliyokolezwa unywe, asali ya maua ya mikomamanga yangu.

3Mkono wake wa kushoto uko chini ya kichwa changu, na mkono wake wa kuume unanikumbatia.

4Binti za Yerusalemu, ninawaagiza: msichochee wala kuamsha mapenzi hata yatakapotaka yenyewe.

5Ni nani huyu anayekuja kutoka nyikani akimwegemea mpenzi wake? Nilikuamsha chini ya mtofaa, huko mama yako alipotunga mimba yako, huko yeye alipata utungu akakuzaa.

6Nitie kama muhuri moyoni mwako, kama muhuri kwenye mkono wako; kwa maana upendo una nguvu kama mauti, wivu wake ni mkatili kama kuzimu. Unachoma kama mwali wa moto, kama mwali mkubwa wa moto wa Bwana hasa.

7Maji mengi hayawezi kuuzimisha upendo, mito haiwezi kuugharikisha. Kama mtu angelitoa mali yote ya nyumbani mwake kwa ajili ya upendo, angelidharauliwa kabisa.

8Tunaye dada mdogo, matiti yake hayajakua bado. Tutafanya nini kwa ajili ya dada yetu wakati atakapokuja kuposwa?

9Kama yeye ni ukuta, tutajenga minara ya fedha juu yake. Na kama yeye ni mlango, tutamzungushia mbao za mierezi.

10Mimi ni ukuta, nayo matiti yangu ni kama minara. Ndivyo ambavyo nimekuwa machoni pake kama yule anayeleta utoshelevu.

11Solomoni alikuwa na shamba la mizabibu huko Baal-Hamoni; alikodisha shamba lake la mizabibu kwa wapangaji. Kila mmoja angeleta kwa ajili ya matunda yake shekeli 1,000 za fedha.

12Lakini shamba langu la mizabibu ambalo ni langu mwenyewe ni langu kutoa; hizo shekeli 1,000 ni kwa ajili yako, ee Solomoni, na shekeli mia mbili ni kwa ajili ya wale wanaotunza matunda yake.

13Wewe ukaaye bustanini pamoja na marafiki mliohudhuria, hebu nisikie sauti yako!

14Njoo, mpenzi wangu, uwe kama swala au kama ayala kijana juu ya milima iliyojaa vikolezo.

Wimbo

Open the interactive reader to switch translations, adjust type, and mark verses — or browse verses by topic.

Neno: Bibilia Takatifu — Kiswahili Contemporary Version. Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. Used under the Biblica Open (Toleo Wazi) License. · Biblica Open License