Wimbo 2
Neno: Kiswahili Contemporary Version
1Mimi ni ua la Sharoni, yungiyungi ya bondeni.
2Kama yungiyungi katikati ya miiba ndivyo alivyo mpenzi wangu katikati ya wanawali.
3Kama mti wa mtofaa miongoni mwa miti ya msituni ndivyo alivyo mpenzi wangu miongoni mwa wanaume vijana. Ninafurahia kuketi kivulini mwa mwanaume huyu, na tunda lake ni tamu kwangu.
4Amenichukua mpaka kwenye ukumbi wa karamu, na bendera ya huyu mwanaume juu yangu ni upendo.
5Nitie nguvu kwa zabibu kavu, niburudishe kwa matofaa, kwa maana ninazimia kwa mapenzi.
6Mkono wake wa kushoto uko chini ya kichwa changu, na mkono wake wa kuume unanikumbatia.
7Binti za Yerusalemu, ninawaagiza kwa paa na kwa ayala wa shambani: Msichochee wala kuamsha mapenzi hata yatakapotaka yenyewe.
8Sikiliza! Mpenzi wangu! Tazama! Huyu hapa anakuja, akirukaruka juu milimani akizunguka juu ya vilima.
9Mpenzi wangu ni kama paa au ayala kijana. Tazama! Anasimama nyuma ya ukuta wetu, akitazama kupitia madirishani, akichungulia kimiani.
10Mpenzi wangu alizungumza na kuniambia, “Inuka, mpenzi wangu, mrembo wangu, tufuatane.
11Tazama! Wakati wa masika umepita, mvua imekwisha na ikapita.
12Maua yanatokea juu ya nchi; majira ya kuimba yamewadia, sauti za njiwa zinasikika katika nchi yetu.
13Mtini unatunga matunda yake ya mwanzoni, zabibu zinazochanua zaeneza harufu nzuri. Inuka, njoo mpenzi wangu. Mrembo wangu, tufuatane.”
14Hua wangu penye nyufa za majabali, mafichoni pembezoni mwa mlima, nionyeshe uso wako, na niisikie sauti yako, kwa maana sauti yako ni tamu, na uso wako unapendeza.
15Tukamatie mbweha, mbweha wale wadogo wanaoharibu mashamba ya mizabibu, mashamba yetu ya mizabibu yaliyochanua.
16Mpenzi wangu ni wangu, nami ni wake, yeye hujilisha katikati ya yungiyungi.
17Mpaka jua linapochomoza, na vivuli vikimbie, rudi, mpenzi wangu, na uwe kama paa, au kama ayala kijana juu ya vilima vya Betheri.
Wimbo
Open the interactive reader to switch translations, adjust type, and mark verses — or browse verses by topic.
Neno: Bibilia Takatifu — Kiswahili Contemporary Version. Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. Used under the Biblica Open (Toleo Wazi) License. · Biblica Open License