Wimbo 3

Neno: Kiswahili Contemporary Version

1Usiku kucha kwenye kitanda changu nilimtafuta yule moyo wangu umpendaye; nilimtafuta, lakini sikumpata.

2Sasa nitaondoka na kuzunguka mjini, katika barabara zake na viwanja; nitamtafuta yule moyo wangu umpendaye. Kwa hiyo nilimtafuta lakini sikumpata.

3Walinzi walinikuta walipokuwa wakizunguka mji. Nikawauliza, “Je, mmemwona yule moyo wangu umpendaye?”

4Kitambo kidogo tu baada ya kuwapita nilimpata yule moyo wangu umpendaye. Nilimshika na sikumwachia aende mpaka nilipomleta katika nyumba ya mama yangu, katika chumba cha yule aliyenichukua mimba.

5Binti za Yerusalemu, ninawaagiza kwa paa na kwa ayala wa shambani: Msichochee wala kuamsha mapenzi hata yatakapotaka yenyewe.

6Ni nani huyu anayekuja kutoka jangwani kama nguzo ya moshi, anayenukia manemane na uvumba iliyotengenezwa kwa vikolezo vyote vya mfanyabiashara?

7Tazama! Ni gari la Solomoni lisindikizwalo na mashujaa sitini, walio wakuu sana wa Israeli,

8wote wamevaa panga, wote wazoefu katika vita, kila mmoja na upanga wake pajani, wamejiandaa kwa ajili ya hofu za usiku.

9Mfalme Solomoni alijitengenezea gari; alilitengeneza kwa mbao kutoka Lebanoni.

10Nguzo zake alizitengeneza kwa fedha, kitako chake kwa dhahabu. Kiti chake kilipambwa kwa zambarau, gari lake likanakshiwa njumu kwa upendo na binti za Yerusalemu.

11Tokeni nje, ninyi binti za Sayuni, mkamtazame Mfalme Solomoni akiwa amevaa taji, taji ambalo mama yake alimvika siku ya arusi yake, siku ambayo moyo wake ulishangilia.

Wimbo

Open the interactive reader to switch translations, adjust type, and mark verses — or browse verses by topic.

Neno: Bibilia Takatifu — Kiswahili Contemporary Version. Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. Used under the Biblica Open (Toleo Wazi) License. · Biblica Open License