Ayubu 4
Neno: Kiswahili Contemporary Version
1Ndipo Elifazi Mtemani akajibu:
2“Kama mtu akithubutu kuzungumza nawe, kutakukasirisha? Lakini ni nani awezaye kujizuia asiseme?
3Fikiri jinsi ambavyo umewafundisha watu wengi, jinsi ambavyo umeitia nguvu mikono iliyokuwa dhaifu.
4Maneno yako yamewategemeza wale waliojikwaa; umeyatia nguvu magoti yaliyokuwa dhaifu.
5Lakini sasa hii taabu imekujia wewe, nawe unashuka moyo; imekupiga wewe, nawe unafadhaika.
6Je, kumcha Mungu kwako hakupaswi kuwa ndiyo matumaini yako na njia zako kutokuwa na lawama ndilo taraja lako?
7“Fikiri sasa: Ni mtu yupi asiye na hatia ambaye aliwahi kuangamia? Ni wapi wanyofu waliwahi kuangamizwa?
8Kwa jinsi ambavyo mimi nimechunguza, wale walimao ubaya na wale hupanda uovu, huvuna hayo hayo hayo.
9Kwa pumzi ya Mungu huangamizwa; kwa mshindo wa hasira zake huangamia.
10Simba anaweza kunguruma na kukoroma, lakini bado meno ya simba mkubwa huvunjika.
11Simba anaweza kuangamia kwa kukosa mawindo, nao wana wa simba jike hutawanyika.
12“Neno lililetwa kwangu kwa siri, masikio yangu yakasikia mnongʼono wake.
13Katikati ya ndoto za kutia wasiwasi wakati wa usiku, hapo usingizi mzito uwapatapo wanadamu,
14hofu na kutetemeka kulinishika na kufanya mifupa yangu yote itetemeke.
15Kuna roho aliyepita mbele ya uso wangu, nazo nywele za mwili wangu zikasimama.
16Yule roho akasimama, lakini sikuweza kutambua kilikuwa kitu gani. Umbo fulani lilisimama mbele ya macho yangu, kukawa na ukimya kisha nikasikia sauti:
17‘Je, binadamu aweza kuwa mwadilifu kuliko Mungu? Je, mtu aweza kuwa safi kuliko Muumba wake?
18Kama Mungu hawaamini watumishi wake, kama yeye huwalaumu malaika zake kwa kukosea,
19ni mara ngapi zaidi wale waishio katika nyumba za udongo wa mfinyanzi, ambazo misingi yake ipo mavumbini, ambao wamepondwa kama nondo!
20Kati ya mawio na machweo huvunjwa vipande vipande; bila yeyote kutambua, huangamia milele.
21Je, kamba za hema yao hazikungʼolewa, hivyo hufa bila hekima?’
Ayubu
Open the interactive reader to switch translations, adjust type, and mark verses — or browse verses by topic.
Neno: Bibilia Takatifu — Kiswahili Contemporary Version. Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. Used under the Biblica Open (Toleo Wazi) License. · Biblica Open License